Skip to content
Tags

Nanchaku

27/03/2014
Cheni za Kupigania

Nanchaku (nunchaku) ni miongoni mwa silaha mbalimbali zilizotumika katika kitabu cha KOLONIA SANTITA: LAANA YA PANTHERA TIGRISI. Silaha hizi zilitumiwa zaidi na magaidi wa Kolonia Santita, dhidi ya Vijana wa Tume katika Msitu wa Benson Bennett.

Advertisements

From → Picha

2 Comments
 1. Kuna hadithi nyingi maarufu ambazo zimekuwa zikisimuliwa katika vitabu vingi huko Okinawa na Japani kuhusiana na nunchaku (nanchaku – Kamusi ya Enock Maregesi), kwamba nanchaku hapo mwanzo ilikuwa mipini ya kuvunia mpunga (au puta), iliyobadilishwa na wakulima wa Kijapani kuwa silaha hatari dhidi ya askari wa tabaka la watawala wa kijeshi wa samurai! Hadithi hizi, hata hivyo, si za kweli katika nyanja zote nne: Nanchaku haijawahi kuwa silaha ya Kijapani, wala haijawahi kutumika kama puta ya kuvunia mpunga. Haikutengenezwa na wanavijiji, wala haikuwahi kutumika dhidi ya askari wa samurai.

  Nanchaku, kama tunavyoijua leo, inatoka katika Kisiwa cha Okinawa huko Uchina … ambayo leo ni sehemu ya Japani. Okinawa ipo takriban katikati ya Taiwani na Japani bara, na ni kisiwa kikubwa kuliko vyote katika mkusanyiko wa visiwa vya Ryukyu (au ‘kamba’), mlolongo wa maili 650 wa visiwa vidogovidogo kati ya Japani Kusini na Taiwani.

  Okinawa ni sehemu ya Japani, lakini Waokinawa si Wajapani, na wanayo lugha na utamaduni wao, ijapokuwa siku hizi lugha yao imemezwa sana na lugha ya Kijapani. Hata hivyo, cha kushangaza ni kwamba, lugha ya Kijapani haina hata neno la nanchaku! Mtu akihitaji kuandika neno ‘nanchaku’ kwa lugha ya Kijapani, anaweza kufanya hivyo kwa njia mbili: Anaweza kutumia mfumo wa alfabeti wa silabi na matamshi wa katakana – unaotumika katika lugha ya Kijapani kuandika maneno ya kigeni na maneno ya mtaani, au maneno ya kihuni – kuandika silabi za neno ‘na-n-cha-ku’. Au, vinginevyo, anaweza kutumia herufi za Kichina za maneno ya double part baton (au virungu viwili); ambayo hutamkwa ‘shuang jie gun’ kwa Kichina, ‘nanchaku’ kwa Kiswahili, ‘nun cha kun’ kwa Kiokinawa na ‘so setsu kon’ kwa Kijapani.

  Watu wengi hudhani kwamba nanchaku ilianza kama puta ya kuvunia mpunga (utzu) katika kipindi cha ukabaila, lakini haya ni makosa. Kupata jibu, hebu fikiria ya kuwa unataka kutumia nanchaku kuvuna mpunga ambao mimea yake umeilaza chini ardhini. Ili kipande cha mkono wa nanchaku kinachoning’inia kitue vizuri kwenye ardhi, lazima utatakiwa kuinama kwa kiasi cha kichwa chako kuwa karibu na magoti yako (au utatakiwa kupiga magoti kwenye ardhi). Kwa staili ya kwanza, kila mara utakapoinama na kuinuka utaweza kupata maumivu ya mgongo; wakati staili ya pili haitakuwa nzuri sana, maana mtu yeyote aliyewahi kufanya hivyo anaweza kukwambia madhara yake ni yapi. Puta halisi ya Kiokinawa, kama ilivyo puta ya Kiulaya, ina mpini mrefu sawa na urefu wa mwanamume ili kazi ya uvunaji iwe rahisi. Hivyo, imani ya kwamba nanchaku inatokana na puta ya Kiokinawa ya kuvunia mpunga ni imani isiyo na msingi hata kidogo. Sababu nyingine ya makosa haya, licha ya mfanano wa waziwazi wa puta za kuvunia mpunga na virungu vya kupigania vya nanchaku, inaweza kuwa uwepo wa magongo ya kupigania (uchibo); ambayo kiukweli ni puta zilizorekebishwa za kuvunia mpunga – miongoni mwa silaha nyingi kadha wa kadha za sanaa ya mapigano za Okinawa ziitwazo kobujutsu.

  Bado ipo mifano zaidi ya imani kali juu ya sampuli kifani (prototype) ya nanchaku. Hata hivyo, imani sadikifu kuliko zote (iliyothibitishwa na baadhi ya wataalamu wa silaha za Kijapani za kobudo, au magongo ya kupigania) ni kwamba nanchaku inatokana na hatamu za farasi ziitwazo muge. Mwanzoni kabisa, mikono ya hatamu ilikuwa imejipinda. Lakini baadaye ilirekebishwa na kuwa silaha iliyonyooka kama inavyojulikana leo.

  Aidha, zipo imani zingine za historia ya nanchaku zisemazo kwamba hapo mwanzo nanchaku zilikuwa njuga za walinzi wa usiku au zana za kukatia mimea ya ndizi (barawaji bora zaidi katika visiwa vya Okinawa hutoka katika gamba la mgomba). Mwishowe, imani nyingine ya mwisho – inayoungwa mkono na wataalamu kama vile wataalamu wa Miyagi na Ikeda wa Japani na Okinawa – inasema kuwa nanchaku iliigwa kutoka katika silaha moja ya Kichina iliyopelekwa Okinawa na wahamiaji wa Kichina. Ushahidi usiokuwa wa moja kwa moja (dhahiri) wa imani hii ni ukweli kwamba, neno linalotumika kwa ajili ya neno ‘nanchaku’ limenakiliwa kutoka katika lugha ya Kichina.

  Historia kwa ufupi ya nanchaku na Okinawa haikuanza mpaka mwanzoni mwa karne ya kumi na tano. Mnamo mwaka 1429, Mfalme Sho Hashi alianzisha himaya ya Sho kwa kuunganisha falme tatu za wana mfalme wa Okinawa: Hokuzan, Nanzan na Chuzan, na hivyo kutengeneza ufalme wa Ryukyu, huku jiji la Shuri likiwa ndiyo mji mkuu wa ufalme. Sho Hashi sasa alikuwa na eneo lililokuwa na muungano wa tawala kadha wa kadha; lakini si nchi moja. Kila mwana mfalme aliishi katika kasri lake na alitawala himaya ya kwake mwenyewe; alikuwa na jeshi la kwake mwenyewe, alikuwa na sheria za kwake mwenyewe za kodi, na alikuwa na mfumo wa kwake mwenyewe wa sheria na mahakama. Mchakato wa kuunganisha hizi falme kuwa nchi moja iliyoungana ulimalizika baada ya takriban miaka 50 iliyofuata, chini ya mmoja wa warithi wa Mfalme Sho Hashi – Mfalme Sho Shin – aliyegeuza ufalme kuwa nchi moja yenye serikali moja, jeshi moja na mfumo mmoja wa sheria, kama zilivyo nchi nyingi za leo.

  Kupunguza uwezekano wa uasi nchini Okinawa, Sho Shin aliwakusanya wana wote wa mfalme (aji) katika mji wa Shuri na kupiga marufuku umilikaji wa silaha. Ni jeshi la mfalme pekee pamoja na malodi walioruhusiwa kumiliki silaha, lakini ni mfalme pekee aliyeruhusiwa kumiliki silaha nyingi kwa wakati mmoja. Matokeo yake, jeshi la mfalme likawa jeshi pekee nchini Okinawa.

  Miaka 180 baadaye – baada ya Mfalme Sho Hashi kuanzisha himaya ya Sho – ufalme wa Ryukyu ambao, mpaka kipindi hicho, ulikuwa bado ni nchi moja huru, ulichukuliwa na dola ya mwana mfalme wa Satzuma wa Japani; na kuwa chini ya miliki ya tawala hiyo mpaka mwaka 1879 ambapo, baada ya mapinduzi ya Meiji, Okinawa ilichukuliwa na Japani. Hata hivyo, katika kipindi chote cha kati ya mwaka 1609 na 1879, uwepo wa Japani nchini Okinawa ulikuwa mdogo! Kulikuwepo na dazani chache tu za askari wa samurai nchi nzima, na wengi wao waliishi katika jiji la Shuri. Serikali ya Japani ilikubaliana na amri ya Sho Shin dhidi ya silaha, na ikaongeza kwa kupiga marufuku uingizaji na umilikaji wa silaha nchini Okinawa hali kadhalika. Hata hivyo, hadithi kuhusu udhibiti hasa wa silaha katika kisiwa cha Okinawa zimebakia kuwa hadithi tu. Watu maarufu wa Okinawa bado waliruhusiwa kumiliki na kubeba mapanga yao, na wanafamilia ya kifalme na wanawafalme walikuwa hata wakiruhusiwa kuwa na bunduki za marisau kwa ajili ya kuwindia.

  Katika vitabu vingi vya kareti, mara nyingi imekuwa ikiandikwa kuwa wakulima ndiyo waliyoanzisha sanaa ya mapigano ya Okinawa. Lakini hii haileti maana yoyote. Okinawa haikuwahi kuwa nchi tajiri na halafu, baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa ajira wa Kijapani katika karne ya 17, Okinawa ilizidi kuwa maskini. Wakulima walilazimika kufanya kazi kuanzia macheo mpaka machweo kwa ajili ya chakula cha familia zao wenyewe. Wanavijiji hawakuwa na muda au hamasa ya kujifunza kupigana na kuendeleza sanaa ya mapigano iliyokuwa bora zaidi.

  Watu maarufu na wenye uwezo ndiyo waliyoanzisha sanaa ya mapigano ya Okinawa. Tabaka la makabaila (kazoku) lilijifunza sanaa ya kupigana, sanasana kama kitu cha kupoteza muda. Lakini kwa tabaka la malodi wafanyakazi (shizoku) maarifa juu ya sanaa ya mapigano kilikuwa kitu cha lazima; kwa vile waliifanyia kazi serikali kama maafisa wa jeshi na polisi, wakusanyaji wa kodi na kadhalika. Tukiangalia nasaba ya mtindo wowote wa kareti au kobujutsu wa Okinawa, tunaona kuwa waanzilishi wa mitindo hiyo ni vitawishina vya familia ya kilodi, au walijifunza sanaa ya mapigano kutoka kwa lodi.

  Lakini, kama kweli sanaa ya mapigano ya Okinawa ilianzishwa na malodi walioruhusiwa kuwa na mikuki na mapanga, kwa nini basi walianzisha mbinu za kupigania miundu, makasia, majembe na vifaa vingine vya wavuvi na wakulima?

  Tabaka la malodi wafanyakazi wa Okinawa (kama unavyoweza kutabiri kutokana na jina lenyewe) waliifanyia kazi serikali kama maafisa wa jeshi na polisi, au maafisa wa serikali. Waliitunza na kuilinda katiba ya nchi yao, na walipata mishahara yao kutoka kwa mfalme. Hawakuwa na vyanzo vingine vya mapato. Sheria iliwabana kufanya kazi za ziada. Hata hivyo, ilifikia kipindi hiyo mishahara waliyokuwa wanapata ikawa haiwatimizii mahitaji yao ya lazima, matokeo yake wengi wao wakageukia wizi na ujambazi uliokubuhu. Mnamo mwaka 1724 (ili kutatua tatizo hili) wafanyakazi wa serikali wakapewa fursa ya kuwa wafanyabiashara, wahunzi na wakulima. Wengi wao waliacha kazi serikalini na walihitaji kuhamia vijijini na familia zao, ili tu waweze kujilisha wenyewe. Baada ya karne moja na nusu, kabla ya mapinduzi ya Meiji, fursa za wafanyakazi wa serikali ya Okinawa pamoja na askari wa samurai wa Japani zilisitishwa (ikiwa ni pamoja na haki ya kumiliki mapanga) na walinyimwa hata mishahara yao. Ukikisoma vizuri kitabu cha Gone With the Wind cha Margaret Mitchell wa Marekani, utakumbuka kisa cha makabaila wa jana waliolazimika kuwa wafanyabiashara wa maduka na waoka mikate ili waweze kuishi. Vivyo hivyo ilitokea hata kwa makabaila wa Okinawa. Wanafamilia ya kifalme walifanya kazi kama wasaisi, watu wanaofanya kazi za kuchunga au kuangalia wanyama wanaopandwa kama vile farasi au punda, na walinzi wa usiku. Wana wafalme walikuwa wakataji wa miti na wauzaji wa nguruwe kwenye masoko. Wafanyakazi wengi wa serikalini walihamia vijijini. Wakulima, bila shaka, wakawa na kinyongo kukutana na majirani wao wapya na kujaribu hata kuwafukuza katika ardhi ya vijiji vyao. Juhudi hizi mara nyingi zilipelekea makundi haya mawili ya watu kupigana. Idadi ya wezi na majambazi kadhalika iliongezeka katika nchi, ambapo chakula kilikuwa ni kitu cha thamani. Matokeo yake, ‘wana-wafalme-wakulima’ walilazimika kufufua ujuzi au weledi wao wa kupigana.

  Tabaka la malodi wafanyakazi wa serikali bila ya shaka, wangependelea kupigana kwa mapanga (au majambia) badala ya kupigana kwa mikono mitupu. Lakini hawakuruhusiwa kuwa na silaha. Hata hivyo, askari hufanya nini anaposhindwa kutumia silaha? Huchukua chochote kinakachokuwa karibu yake. Watawa wa Shaolin walivumbua mbinu za kupigana kwa ndala na vikapu, huku maninja wa Japani wakijifunza kuua wapinzani wao kwa vijiti vya kulia chakula. Tabaka la malodi wafanyakazi wa Okinawa, wakiwa hawaruhusiwa kumiliki silaha, hali kadhalika walivumbua silaha kutokana na kitu chochote walichoweza kupata.

  Fimbo na vitu mbalimbali vyenye marefu tofauti (rokushakubo yenye urefu wa futi sita, jo futi nne, hanbo futi tatu, nk.) siku zote zilitumika kama silaha za ziada, hivyo zilitumika kwanza. Miundu (kama), makasia (eku), majembe (kuwa), ndoana (nunt-bo), mawe ya kusagia (tonfa) na vifaa vingine vilivyoonekana kuwa vizuri zaidi katika ugomvi kadhalika havikusahalika. Fimbo mbili zilizounganishwa kwa kamba zilivutia macho ya mtu fulani. Shujaa mmoja alizizungusha, halafu akapata picha kichwani mwake yule shujaa akimpiga adui kichwani – na nanchaku ikazaliwa.

  Nanchaku haikuwa silaha maarufu miongoni mwa silaha zingine huko Japani na Okinawa. Tumelihitimisha hili kwa sababu hakuna mtindo wowote wa kienyeji wa nanchaku unaojulikana leo. Kinyume chake, leo tunajua kata (staili) nyingi za kale za silaha za kienyeji. Pengine ukosefu wa umaarufu wa nanchaku ulitokana na uwezo wake mdogo wa kufanya kazi pale ilipolinganishwa na silaha zingine za kienyeji ukiachilia mbali upanga. Kwa upande mwingine, mtu aliyekuwa na utaalamu wa matumizi ya nanchaku alikuwa na uwezo mkubwa wa kuwashinda wapinzani wachache waliokuwa na visu au waliokuwa hawana silaha yoyote. Aidha, nanchaku ilikuwa rahisi kufichika. Watu walikuwa wakitembea nayo kila siku. Hivyo, huko Okinawa, zaidi nanchaku ilikuwa ikitumika kama silaha ya mtaani ya kujilindia dhidi ya watu wakorofi na majambazi.

  Silaha kama nanchaku zinapatikana katika mifumo ya sanaa nyingi za mapigano duniani kote. Mifano michache ya silaha bora zinazofanana na nanchaku ni kama vile erjiegun ya Kichina, tabak-toyok ya Filipino, ssangjulbong ya Korea, na puta za kupigania za bara la Ulaya. Silaha (zote) hizi zinatengenezwa kama nanchaku. Baadhi yazo ni nanchaku zilizotengenezwa kutokana na silaha za asili za Japani na Okinawa ziitwazo kobudo. Chako ya Filipino na tabak-toyok kwa mfano, hazina tofauti yoyote na nanchaku za Okinawa: zilizotengenezwa kutokana na mbao au miti ya Filipino. Hata hivyo, sanaa zingine za mapigano zina aina zake zenyewe za ‘silaha za minyororo’, kama sanjiegun ya Shaolin au mipini ya kupigania ya bara la Ulaya…

  Lakini leo nanchaku ni maarufu sana – kiasi kwamba karibu kila aina mpya ya sanaa ya mapigano hutumia nanchaku katika programu zake za mazoezi. Kutokana na urahisi wa upatikanaji wa malighafi na urahisi wake wa kutengeneza, uwezo wake mkubwa wa upiganaji wa mtaani na umaarufu wake kuongezeka kutokana na sinema za Bruce Lee, nanchaku imezaliwa upya katika nyakati za leo. Nanchaku, leo, ni miongoni mwa silaha maarufu sana baada ya kisu na kirungu.

  Habari hii imetafsiriwa (kutoka kwa Alex Levitas) na Enock Maregesi.

 2. hans ramadhani permalink

  very nice

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: