Skip to content

Sheria ya Siku ya Sabato

31/10/2016

197. Sabato ilianzishwa na Mungu siku ya saba ya uumbaji wake. Siku ya Sabato ni siku takatifu, iliyoko katika Amri Kumi za Mungu, ambayo hatuna budi kuitunza na kuiheshimu. Sheria ya Siku ya Sabato haikufa baada ya kifo cha Yesu Kristo msalabani kama Wakolosai wanavyodai. Wakolosai walifuata falsafa za kipagani, na walizileta falsafa hizo ndani ya mwili wa Kristo ambalo ni kanisa. ‘Usiiamini’ Wakolosai 2:17. Iamini Wakolosai 2:20-23, ambapo Paulo anafundisha Mataifa jinsi ya kuitunza Sabato, na 1 Wakorintho 12:27 ambayo inatoa maana halisi ya Wakolosai 2:17. ‘Mwili wako ni wa Kristo’ ni tofauti na ‘mwili wa Kristo’ na ni tofauti na kanisa. Ukiamini kama mwili wako ni wa Kristo na ni kanisa, utaitunza Sabato.

Kumbukumbu la Torati 5:12-15 inasema, “Ishike siku ya Sabato uitakase, kama BWANA, Mungu wako, alivyokuamuru. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya BWANA, Mungu wako; siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala ng’ombe wako, wala punda wako, wala mnyama wako ye yote, wala mgeni aliye ndani ya malango yako, ili mtumwa wako na mjakazi wako wapumzike vile vile kama wewe. Nawe utakumbuka ya kuwa wewe ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, na ya kuwa BWANA, Mungu wako, alikutoa huko kwa mkono wenye nguvu, na mkono ulionyooshwa; kwa sababu hiyo BWANA, Mungu wako, akikuamuru uishike Sabato.”

Tazama jinsi tunavyoamrishwa kuitakasa Sabato. Msisitizo hapa ni katika suala la uhuru. Mungu anasema, “Nawe utakumbuka ya kuwa ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri,” Kidokezo hiki kiko wazi! Wana wa Israeli walipokuwa watumwa, hawakuwa na uhuru hata wa kujiamulia mambo yao wenyewe. Kwa hiyo, iwapo tutaitunza Sabato kama vile inavyotakiwa, tutakuwa huru. Iwapo itatumika vizuri, Sabato itatushurutisha kukumbuka siku za nyuma; sawa tu na itakavyotushurutisha kukumbusha siku za mbele, kule maisha yetu yanapoelekea.

Tutafanya hivyo kwa kujifunza Biblia na kusikiliza sauti ya Roho Mtakatifu; ujumbe ambao utatuhamasisha, pamoja na taamuli na mazungumzo ndani ya ushirika. Katika ibada za kanisani, tunasikia mengi juu ya Ufalme wa Mungu na juu ya dunia ya leo. Ibada nyingi uhusisha dhambi kwa namna fulani. Dhambi ni uvunjaji wa sheria (1 Yohana 3:4), lakini Amri Kumi za Mungu ni sheria ya uhuru (Yakobo 1:25). Kwa kuzitunza amri hizo tutabaki kuwa huru dhidi ya utumwa wa Shetani, dunia hii, na hata kifo. Katika siku ya Sabato, Mungu huelekeza watu wake kupitia Neno lake juu ya jinsi ya kuzitunza amri zake na hivyo kubaki huru. Kutoka 16:4, 25-30 inaeleza zaidi:

Ndipo BWANA akamwambia Musa, “Tazama, mimi nitawanyeshea ninyi mvua ya mkate kutoka mbinguni; na hao watu watatoka nje na kuokota kila siku sehemu ya siku; ili nipate kuwajaribu, kwamba watakwenda katika sheria yangu, ama sivyo.” … Kisha Musa akasema, “Haya, kuleni hiki leo; kwa kuwa leo ni Sabato ya BWANA; leo hamtakiona nje barani. Siku sita mtaokota; lakini siku ya saba ni Sabato, siku hiyo hakitapatikana.” Ikawa siku ya saba wengine wakatoka kwenda kukiokota, wasikione. BWANA akamwambia Musa, “Mtakataa kuyashika maagizo yangu na sheria yangu hata lini? Angalieni, kwa kuwa BWANA amewapa ninyi hiyo Sabato, kwa sababu hii huwapa siku ya sita chakula cha siku mbili; kaeni kila mtu mahali pake, mtu awaye yote asiondoke mahali pake kwa siku ya saba.” Basi hao watu wakapumzika kwa siku ya saba.

Amri ya kwanza kabisa ambayo Mungu aliwafunulia Wana wa Israeli baada ya kuwakomboa kutoka utumwani ilikuwa ni ile iliyokuwa na dhamira ya kuwaweka huru, yaani Sabato. Mungu aliwapa ushuhuda huu wa chakula cha maajabu cha siku mbili cha mana, katika siku ya sita, bila kuwapa chochote katika siku ya saba, kwa muda wa miaka arobaini! Kinyume cha wale wanaodai kuwa Sabato imebatilishwa au imebadilishwa, Sabato ni zawadi ya ajabu kutoka kwa Mungu.

Kwa karne nyingi, watu wamejaribu kutafuta njia za kujishawishi wenyewe na kuwashawishi wengine kwamba Wakristo hawatakiwi kutunza Sabato na siku takatifu. Mojawapo ya mafungu wanayoyapenda zaidi katika harakati zao hizo ni Wakolosai 2:16-17. Baadhi hufundisha ya kwamba, kundi la uasi la Wayahudi katika kanisa la Kolosai lilikuwa likijaribu kutekeleza utii kwa tamaduni za Kiyahudi; kama vile sheria za nyama safi na najisi na za kutunza siku takatifu. Chini ya mazingira kama hayo, wanasema, Paulo anawaambia Wakolosai ya kwamba hawakuwa na haja ya kuwa na wasiwasi juu ya kile wengine walikuwa wakihukumu na kusema kuhusu wao.

Upindishwaji wa sehemu hii ya maandiko kwa kiasi fulani huanza kwa kutokuielewa vizuri Wakolosai 2:14, jambo ambalo wengi huthibitisha kwamba sheria iliondolewa na kugongomewa misumari msalabani. Wanaamini kwamba Paulo anasema katika fungu la 16, “Basi [kwa vile sheria imeondolewa], mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au Sabato.” Kwa hiyo, hutafsiri mstari wa 17 kumaanisha kwamba Paulo anakanusha Sabato na siku takatifu kirahisi kama ishara zisizo muhimu za matukio yajayo; huku wakisisitiza kuwa, haja pekee ya kweli ya Mkristo wa kweli ni imani katika Kristo. Kutokana na hili, wanahitimisha kwamba hatupaswi kuwa na wasiwasi kutokana na hizi siku takatifu kwa sababu, kwa kuwa Kristo alikufa, maadhimisho yake hayatakiwi tena.

Paulo anasema nini hasa katika mafungu haya ambayo aghalabu hueleweka vibaya? Kuyaelewa maandiko haya vizuri lazima kwanza tuufikirie usuli wa kiutamaduni na kihistoria wa watu ambao Paulo alikuwa akiwaandikia. Wakolosai walikuwa wameathiriwa kwa kiasi kikubwa na falsafa za kipagani, ambazo zilifundisha kuwa ukamilifu uliweza kupatikana kwa njia ya kujinyima na kujiepusha na anasa. Matokeo yake, Kolosai ikawa jumuiya ya kujiepusha na raha na anasa ambayo ilizingatia utawala wa dini, wananchi wake wakadhani mtu yoyote aliyekuwa na dini alipaswa kuishi kama walivyoishi wao.

Wengi wa watu waliobadilisha imani zao na kuwa Wakristo walikuja kanisani na falsafa zao za kipagani, na baadaye wakaanza kuwa na ushawishi mbaya juu ya Wakristo wote wa huko Kolosai. Paulo anawasahihisha Wakristo waliokuwa wanafanya hivyo katika Wakolosai 2:20-23:

“Basi ikiwa mlikufa pamoja na Kristo mkayaacha yale mafundisho ya awali ya ulimwengu, kwa nini kujitia chini ya amri, kama wenye kuishi duniani, Msishike, msionje, msiguse; (mambo hayo yote uharibika wakati wa kutumiwa); hali mkifuata maagizo na mafundisho ya wanadamu? Mambo hayo yanaonekana kana kwamba yana hekima, katika namna ya ibada mliyojitungia wenyewe, na katika kunyenyekea, na katika kuutawala mwili kwa ukali; lakini hayafai kitu kwa kuzizuia tamaa za mwili.”

Inavyoonekana, baadhi ya watu walishaanza kufikiria kwamba kujinyima huko kwa raha na anasa waliojitwisha kungeweza kwa kiasi fulani kuchangia kwenye wokovu wao na walishaanza kuwa na mtazamo tofauti dhidi ya Yesu Kristo. Walikuwa na imani zaidi katika kazi zao za kipagani. Paulo aliwaonya kuhusu hili katika Wakolosai 2:8: “Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo.”

Mungu alishawaita watu katika kanisa la Kolosai waachane na tamaduni zao za kipagani, na walishaanza kujifunza jinsi ya kufurahia maisha kwa namna ya uwiano kama Mungu alivyokusudia. Hii ilikuwa ni pamoja na kula nyama, kunywa divai, na kufurahia chakula na ushirika, huku wakitunza Sabato ya Mungu na sherehe zake. Inavyoonekana watu walifurahia kukutana pamoja na kushirikiana kwa kiasi cha hata wengine kusherehekea miezi mipya, sikukuu ambazo Mungu hakutaka zifanyike lakini, ambazo zilishakuwa tamaduni chini ya Agano la Kale.

Kwa vile wale Wakolosai walioongoka walikuwa wakijifunza jinsi ya kuyafurahia maisha kama Mungu alivyokusudia, watu nje ya kanisa walianza kuwaonea gere na kuwashutumu. Katika kushughulikia matatizo haya, Paulo anawakumbusha Wakolosai ya kuwa wamekamilika katika Yesu Kristo; hawana haja tena ya falsafa za kipagani za dunia hii. “Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili. Na ninyi mmetimilika katika yeye aliye kichwa cha enzi yote na mamlaka.” Wakolosai 2:9-10.

Katika mistari ya 11 na 14, Paulo anaonyesha jinsi Yesu Kristo alivyokufa kulipa adhabu kwa ajili ya dhambi zetu na sasa dhambi zetu zilizopita; zilizotokana na kufuata njia, tamaduni, na falsafa za dunia hii, zilivyo na kasoro na zilivyogongomewa msalabani kwake. Anawakumbusha ya kuwa Kristo ameshawashinda kabisa roho wote wabaya wanaoendelea kutawala ulimwengu huu mbaya wa sasa, na ambao uhamasisha falsafa za kipagani zilizokuwa zikitawala katika jamii ya Kolosai: “Akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.” (mstari wa 15).

Kwa maneno hayo yenye nguvu na ya kutia moyo kama usuli, Paulo anaelekeza katika mstari wa 16 kwa nini Wakristo wa kipindi hicho hawakupaswa kuwa na wasiwasi dhidi ya tabia ya jamii ya Kolosai juu ya desturi zao na maisha mapya ya kanisa:

“Basi [Kwa kuwa Yesu Kristo ni Bwana na Mwalimu wenu na ameshinda na ana mamlaka juu ya nguvu zote za giza katika dunia hii], mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato.”

Kwa maneno mengine, msiwe na wasiwasi juu ya nini watu katika jamii hufikiri juu ya starehe yenu ya kula chakula kilicho bora, kunywa divai, na kuadhimisha Sabato na siku takatifu kwa furaha. Kristo ameishinda dunia na watawala wake wote, hivyo hatuna haja ya kuwa na wasiwasi kuhusu nini dunia inasema kuhusu sisi.

Katika mstari wa 17, Paulo anataja kwamba Sabato na sikukuu takatifu ni ‘kivuli’ – ishara au aina fulani ya mambo yajayo katika mpango wa Mungu. Sabato ni aina ya Milenia ambapo Yesu Kristo na watakatifu watatawala dunia kwa miaka elfu moja. Siku takatifu huashiria hatua mbalimbali katika mpango wa Mungu, na hutukumbusha kila mwaka kusudi kuu la Mungu katika uumbaji wa mwanadamu.

Maneno ya mwisho katika mstari wa 17 – “bali mwili ni wa Kristo.” – ni tafsiri mbaya iliyotokana na kushindwa kuelewa maana halisi ya kile ambacho Paulo alikuwa akikisema. Huo ni mfano bora wa jinsi watafsiri wakati mwingine wanavyoitafsiri Biblia pale wanapotafsiri Kigiriki cha awali kwenda katika lugha ya Kiingereza, na hivyo kwenda katika lugha zingine.

Tafsiri halisi ya maneno ya mwisho ya Wakolosai 2:17 inasema, “bali mwili wako ni wa Kristo.” Lakini mwili wa Kristo ni nini? 1 Wakorintho 12:27 inatupatia jibu: “Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake.” Mwili wa Kristo ni kanisa! Nukuu halisi ya Kigiriki inayofanana kabisa na tafsiri ya “mwili wa Kristo” katika 1 Wakorintho 12:27 (‘soma Christou’) imetumika katika Wakolosai 2:17.

Maana kamili sasa ya kile Paulo alichokuwa akikisema inajidhihirisha wazi! Anawaambia Wakolosai kwamba hawapaswi kuruhusu mtu yoyote kuwahukumu au kuwauliza maswali juu ya mambo haya bali waache kanisa lifanye maamuzi hayo. Anawaelekeza wafuasi wake kwenye mfano wa viongozi wa kiroho wa kanisa ambao walijenga msingi na kuweka utaratibu wa kuabudu katika siku ya Sabato na katika siku takatifu, akiwasihi wasiwe na wasiwasi kuhusu mtu yoyote katika jamii anasema nini kuhusu wao. Ushawishi kama huo unatolewa katika mistari ya 18 na 19:

“Mtu asiwanyang’anye thawabu yenu, kwa kunyenyekea kwa mapenzi yake mwenyewe tu, na kuabudu malaika, akijitia katika maono yake na kujivuna bure, kwa akili zake za kimwili; wala hakishiki kichwa, ambacho kwa yeye mwili wote ukiruzukiwa na kuungamanishwa kwa viungo na mishipa, hukua kwa maongeo yatokayo kwa Mungu.”

Katika mafungu haya, Paulo kwa mara nyingine anawatahadharisha Wakolosai kwamba hawapaswi kuruhusu shinikizo la jamii ambamo waliishi kuwa na ushawishi wowote juu ya imani zao na tamaduni zao na anaendelea kuwasihi walitegemee kanisa pekee kwa ajili ya chakula chao cha kiroho na ustawi wa maisha yao.

Hivyo basi, tunaona kwamba, mbali na kuibatilisha Sabato na siku takatifu, Wakolosai 2:16-17 ni ushahidi tosha kwamba kanisa la awali lilizitunza siku hizi na kwamba Paulo alifundisha Mataifa jinsi ya kuzitunza.

One Comment
  1. Paulo, mtumishi wa Bwana aliyefanya kazi kubwa zaidi ya Mungu kuliko mitume wote, alikuwa akiongea na Wakolosai katika ‘lugha’ waliyoielewa.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: