Skip to content
Tags

IJUE DAWA YA KULEVYA YA HEROINI KWA UNDANI ZAIDI. BIASHARA KUU YA PILI YA KOLONIA SANTITA BAADA YA KOKEINI, ILIYOMFANYA PANTHERA TIGRISI AWE TAJIRI WA KUTUPWA KATIKA MIAKA YA 80

22/12/2016

heroini

Heroini hutokana na mmea wa maua uitwao mbaruti-afyuni, ‘oppium poppy’, jamii ya mimea ya mibaruti (‘poppy’) inayopatikana katika sehemu mbalimbali za dunia hususan katika bara la Asia. Mbaruti-afyuni ni mmea mrefu wenye kirungu kidogo kwa juu kama tunda hivi, lenye maua kidogo kwa juu yake. Tunda hilo ambalo hujulikana kama tumba au jicho la ua au ‘poppy pod’ au ‘bud’ kwa utaalamu zaidi, linapokomaa hupasuka na kutoa maua mazuri mekundu ambayo baadaye hutumika kama mapambo katika nyumba za watu.

Licha ya kutumika kama mapambo katika nyumba za watu na katika sherehe mbalimbali za kimila, mbaruti-afyuni hutumika kwa kutengenezea chakula na madawa ya kulevya hali kadhalika; kwa sababu za kiuchumi na kiutabibu. Kabla tunda halijaiva na kupasuka, wakulima – kwa kutumia nyembe maalumu – hulikata kwa kulichanja na kutoa afyuni (au utomvu au kasumba au ‘latex sap’ au ‘opium’) au ‘machozi ya mbaruti’.

Ndani ya afyuni (utomvu unaotumika kutengenezea heroini) kuna asilimia 12 ya morfini na kemikali zingine za kialkaloidi zinazojulikana kitaalamu kama ‘opiates’, kama vile thebaini (‘paramorphine’) na kodini (‘3-methylmorphine’). Morfini hiyo baadaye hushughulikiwa kikemia na kutengeneza heroini na madawa mengine kwa ajili ya sayansi na utabibu. Kwa hiyo afyuni inatengeneza morfini na morfini inatengeneza heroini.

Aidha, baada ya kutoa afyuni yote ama kwa mikono au kwa mashine, tunda hupasuliwa na kutoa mbegu nyingi ndogondogo zilizokuwemo ndani. Mbegu hizo zenye mafuta huweza kuliwa kama chakula, au huweza kukamuliwa na kutoa mafuta kwa ajili ya kupikia na kwa ajili ya matumizi mengine.

Afyuni huzalishwa katika maeneo manne tu ya dunia nzima: Afuganistani, Kusini-Mashariki mwa Asia – ikiwemo Bama na Tailandi, Amerika ya Kusini hasa Kolombia, na Sinaloa nchini Meksiko. Afuganistani ndiyo inayoongoza duniani kwa kuzalisha afyuni, kuliko nchi nyingine yoyote ile, ikiwa imefikia hadi kiwango cha asilimia 90.

Kutengeneza heroini si kazi ngumu hata kidogo. Unachohitaji ni kemikali tu za kawaida pamoja na maji mengi. Baada ya kuvunwa, afyuni huchemshwa na chokaa au kalisi na kutengeneza morfini inayoweza kuyeyushwa na maji. Kisha morfini hiyo huchujwa na kuchemshwa tena, lakini sasa na madini ya shabu, ili kupata morfini ya poda iliyokauka. Mamafia hupakia poda hiyo katika vifurushi na kuipeleka katika maabara za mafichoni katika milima ya Afuganistani, ambako morfini hushughulikiwa kitaalamu na kutengeneza heroini. Kutoka Afuganistani heroini husafirishwa mpaka Irani na Pakistani. Huko husafirishwa kwa njia ya anga, maji na ardhi; mpaka Urusi, Ulaya ya Mashariki, Uturuki, China na Afrika ya Magharibi. Uturuki na Afrika ya Magharibi ni vituo vikuu vya usafirishaji wa madawa yanayokwenda Afrika, Ulaya na mabara yote ya Amerika.

Chokaa ni ‘slaked lime’, kalisi ni ‘calcium’ lakini kalisi inayotengeneza heroini ni ‘calcium hydroxide’; na madini ya shabu ni ‘ammonium chloride’.

Mtumiaji wa heroini huweza kuivuta kwa mdomo, kwa pua, kwa kujidunga kwa sindano katika mishipa ya damu au kwa kujidunga kwa sindano katika sehemu za siri. Wale wanaochanganya bangi na heroini huwa wanavuta heroini kwanza kwa msokoto wa bangi, ambao haujawashwa, kisha, baada ya heroini kwisha, ndipo wanawasha msokoto na kuvuta bangi kama sigara ya kawaida. Hivyo, heroini haivutwi kama sigara.

Sindano katika vena inalewesha kwa ufanisi zaidi kuliko njia zingine za utumiaji wa heroini. Njia ya pili kwa ufanisi ni njia ya sehemu za siri ikifuatiwa na kuchemua. Sindano huchukua sekunde chache kumlewesha mtu, wakati kuvuta kwa pua (kuchemua) huchukua mpaka dakika 15. Mtu anapojidunga heroini, heroini husafiri katika mkondo wa damu hapohapo na kupenya kinga ya damu na ubongo kichwani. Inapoingia katika ubongo heroini hubadilika kikemia na kuwa morfini, na kufurika katika sehemu yote ya mfumo wa ubongo inayoshughulika na furaha, na kumfanya mtumiaji ajisikie raha ya kupindukia. Tabia hiyo ikiendelezwa kwa muda mrefu heroini hubadili muundo na kazi ya ubongo na kumwingiza mtumiaji katika utegemezi na uraibu usio na kifani wa madawa ya kulevya. Ukishakuwa teja umejitia kifungoni. Usipo’kita’ (usipo’fix’), usipopata dozi ya heroini, utaugua kitu kinaitwa ‘ugonjwa wa heroini’ (au ‘dope sickness’). Utajisikia homa, kutetemeka, kutapika na maumivu ya misuli.

Ma Nang Nyi, binti mpendwa wa Kamishna-mlezi wa Kanda ya Asia-Australia ya Tume ya Dunia ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya U Nanda, alipojidunga sindano ya heroini na kuzidisha dozi bila kujua huko Bama, alianza kufifia na kuishiwa na nguvu. Kiasi kikubwa cha heroini kinapofurika katika ubongo wa mtumiaji mfumo wa kupumua huathirika kwa kiasi kikubwa na mwili husahau kupumua. Mtumiaji anakuwa mahututi. Asipofanyiwa huduma ya kwanza haraka, heroini itashinda vita na moyo wake utasimama kupiga.

Miaka miwili baadaye, baada ya Nang Nyi kufa kwa kuzidisha dozi ya heroini bila kujua huko Rangoon; mpenzi wake (Ko San Pe) alipelekwa katika kliniki ngumu kuliko zote duniani ya Tham Krabot, inayomilikiwa na watawa katika milima ya Tailandi, kwa ajili ya tiba ya heroini na ulevi sugu wa pombe. Lakini mwaka 1982 naye akafariki dunia, kama mpenzi wake Ma Nang Nyi. Hiyo ikawa sababu ya U Nanda kuisaliti KGB na kujiunga na Tume ya Dunia ili apambane na madawa ya kulevya kwa nguvu zake zote.

Watumiaji wengi wa heroini huanza na dawa za kupunguza maumivu kama vile ‘oxycodone’ (‘oxys’) ambazo hupatikana kwa wingi katika maduka ya dawa. Miezi minne hivi daktari anapositisha utoaji wa ‘oxys’ kwa mgonjwa, mgonjwa anakuwa tegemezi wa dawa hizo na kujenga uraibu. Mgonjwa anaposhindwa kupata dawa hizo kihalali kwa maagizo ya daktari huzipata kwa walanguzi wa mitaani na kuzinunua, lakini kwa bei ya juu.

Kidonge kimoja cha ‘oxys’ huuzwa kwa Tsh. 120,000 mpaka Tsh. 200,000 na mtu huweza kutumia hata vidonge vitano kwa siku. Uraibu wa ‘oxys’ unapoongezeka, na mgonjwa hana tena hela ya kununulia vidonge, mgonjwa uhamia katika kuiba kwa ndugu, jamaa na marafiki kukidhi haja ya ‘oxycodone’. Huko Marekani kumekuwa na matukio mengi ya watu kuvamia maduka ya dawa na kuiba ‘oxys’ kwa unyang’anyi; na hivyo wengi kukamatwa na kushtakiwa na kufungwa jela.

Tofauti kati ya ‘oxycodone’ na heroini ni kwamba heroini hupatikana kwa urahisi, ina nguvu zaidi, na hugharimu kiasi kidogo tu cha pesa. Hata hivyo, zote hizo zina madhara sawa katika ubongo na uridhishaji wake hautofautiani. Kadiri utakavyotumia ndivyo utakavyohitaji na ndivyo utakavyoumia.

Morfini, thebaini na kodini ni alkaloidi zinazopatikana ndani ya afyuni – kutoka kwenye mmea unaojulikana kitaalamu kama ‘Papaver somniferum’. Kwa jumla hujulikana kama ‘opiates’. Morfini hutengeneza heroini, thebaini hutengeneza ‘oxycodone’, kodini hutengeneza ‘naproxen’ ambayo ni dawa ya homa. Heroini hubadilikia ndani ya ubongo kuwa morfini, wakati kodini hubadilikia ndani ya ini kuwa morfini hali kadhalika.

Watu hutumia vibaya ‘opiates’ kuliko kokeini, eksitasi na methi kwa pamoja. ‘Opiates’ zingine ni kama ‘hydrocodone’ (ambayo ni dawa ya maumivu), ‘xanax’ (ambayo ni dawa ya msongo wa mawazo) na ‘percocet’ (ambayo pia ni dawa ya maumivu).

Uraibu wa heroini si rahisi kupona katika kliniki za kawaida. Watu walioathiriwa na dawa hiyo wanapaswa kujaribu kupelekwa katika kliniki bora zaidi kama vile Betty Ford Center (iliyoko Rancho Mirage, California, inayojihusisha zaidi na ulevi sugu wa pombe) au Tham Krabok ambapo waathirika huishi kama watawa na kutumia dawa za ajabu kwa muda wa majuma manne mfululizo, ambapo kila mtawaliwa lazima ale kiapo cha ‘sajja’ (nadhiri) kabla ya kuanza matibabu. Unaambiwa na mkuu wa watawa uachane kabisa na dawa za kulevya. Hutakiwi kuvunja kiapo hicho hadi mwisho wa matibabu yako.

Watawaliwa wengi wa madawa ya kulevya katika nyumba ya Tham Krabot (iliyoko Saraburi, Tailandi) huwa hawamalizi dozi, kwa sababu ya ugumu wa dozi yenyewe na ugumu wa maisha kwa jumla. Lakini ukimaliza dozi LAZIMA upone.

Kadiri unavyozidi kupanda juu ndivyo utavyoanguka vibaya. Kadiri unavyozidi kutumia madawa ya kulevya ndivyo madhara yake yatakavyokuwa makubwa. Hivyo acha, wakati bado mapema.

 

From → Picha

Leave a Comment

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: