Skip to content

UHAKIKI WA KITABU CHA HUMAN POACHERS CHA ELIAS MUTANI

10/03/2017

Human Poachers

Master Lwanga na Joan ni mashujaa waliookoa maisha ya Jasiri, kijana mdogo mwenye ulemavu wa ngozi, katika kijiji cha kufikirika cha Saanane kilichoko mkoani Shinyanga. Lakini Lwanga na Joan hawakuwa peke yao. Walisaidiwa na watu wengi wakiwemo wanafunzi, walimu, wanakijiji, dereva wa teksi, na jeshi la polisi la Mkoa wa Shinyanga.

Kutokana na juhudi za watu wote hawa maisha ya Jasiri yalibadilika kichanya, huku ya msaliti mkuu wa watu wa Saanane mwenyekiti wa kijiji yakibadilika kihasi.

Human Poachers inatufundisha mambo mengi. Inatupa maarifa kuhusu ulemavu wa ngozi na dhana potofu zinazojitokeza kutokana na ulemevu huo. Vilevile inatufundisha kuwa kumbe mbinu za kiskauti zinaweza kusaidia kutatua matatizo sugu yanayolikumba taifa letu kwa kuzifundisha hasa vijijini ambako tatizo la ulemavu wa ngozi limekithiri. Inatufundisha pia ushirikiano, na inatufundisha jinsi ya kuandika vizuri.

Hata hivyo, kama ilivyo hadithi nyingine yoyote, Human Poachers ina mapungufu yake. Hatujui kwa mfano lugha waliyokuwa wakitumia watu wa Saanane. Hatujui kama walikuwa wakitumia Kiswahili, Kisukuma, Kiingereza, lugha yao wenyewe kwa vile Saanane ni kijiji cha kufikirika, au zote kwa pamoja.

Hatujui muda hasa wa mandhari ya hadithi licha ya kujua ilitokea katika kizazi hiki, ambapo tunaona hata baadhi ya wahusika wakiwa na simu za mikononi.

Aidha, kwangu mimi sikuupenda sana mwisho wa hadithi. Ningependa hadithi iishe kwa furaha au huzuni lakini wale wote wabaya wafikishwe katika vyombo vya dola kujibu mashtaka yaliyowakabili.

Wale wauaji wawili ambao Joan na Jasiri kwa nyakati tofauti waliwaona msituni wakijadiliana jinsi ya kumteka nyara Jasiri na kutengeneza pesa kutokana na viungo vya mwili wake, ijapokuwa yule mrefu hatujui kama alikufa au alizimia baada ya kupigwa na Joan na hata yule mfupi ambaye naye hatujui kama alikufa au alizimia baada ya kupigwa na Sunga, kadhalika ningependa kuona wakiadabishwa mahakamani.

Watu kama wale waheshimiwa wanasiasa wa Shinyanga waliokuwa wakivitaka viungo vya mwili wa Jasiri ili wapate pesa na madaraka, na hata mwenyekiti wa kijiji ambaye katika sura ya kumi alipotea nyumbani kwake alfajiri na hatukumwona tena hadi aliposhushwa na gari la mheshimiwa mmoja katika pango la Kilimanjaro, nao ningependa kuona wakiadabishwa.

Mwenyekiti wa kijiji asingeruhusiwa kufa. Angebakishwa hai ili ajibu mashtaka yote yaliyomkabili, na ataje wale wote waliohusika na mtandao wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, ili liwe fundisho kwa wananchi wote.

Pikipiki aliyochukua Joan na Omari kuwafukuzia majambazi ilitokea ghafla mno. Palitakiwa pawepo na kitu kinachoitwa foreshadowing, kitu ambacho kingetuonyesha kabla kwamba Joan na Omari wangekutana na msaada wa pikipiki ambayo ingewasaidia kumwokoa Jasiri.

Lugha katika ukurasa wa sabini na saba imekosewa kidogo. Badala ya “Do not return it to me” imeandikwa “Do not to return it to me”. Mhusika anaruhusiwa kukosea. Kwani katika mazungumzo ya kawaida watu hukosea. Lakini sidhani kama Joan alizungumza hivyo kwa makusudi alipokuwa akimkabidhi Salu kipenga.

Makosa haya hata kwenye kitabu changu Kolonia Santita yapo. Lakini si busara kwa makampuni ya uchapishaji kufanya makosa ya wazi kama hayo.

Licha ya makosa hayo madogomadogo hadithi ya Human Poachers ni hadithi nzuri sana, na Mwandishi Elias Mutani ni mwandishi bora. Ni rahisi kujua kwa nini kitabu hiki kilishinda Tuzo ya Burt mwaka 2016. Kwa sababu kimeandikwa kwa utaalamu na weledi wa hali ya juu na mwandishi ameunganisha vyema ubunifu, taharuki na uhalisia. Lakini swali langu ni moja: Master Lwanga ndiye Elias Mutani?

Serikali yetu isikie. Labda mbinu za kiskauti zilizotumika katika kitabu hiki zitasaidia kutokomeza tatizo la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi Tanzania.

Save

Advertisements

From → Mengineyo

Leave a Comment

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: