Skip to content

Dawa ya Uchawi ni Wema

07/08/2017

Wema

237. Dawa ya uchawi ni wema. Ingia ndani ya kichwa chako kuujua ukweli.
 
Mpende adui yako ili aone aibu ya kukufanyia ubaya. Huo ndiyo ukweli. Tumia akili yako kuujua ukweli.
 
Mwaka 1922 katika Kisiwa cha Kaguru, Kijiji cha Bugwema, Kata ya Murangi, Tarafa ya Nyanja (Majita), Wilaya ya Musoma Vijijini, Mkoa wa Mara, aliishi dada mmoja mwema sana. Jina lake aliitwa Nyabujoli Manani. Dada huyu alipendwa sana na idadi kubwa ya watu hapo kijijini, na hata katika vijiji vingine vya jirani.
 
Jirani na nyumba aliyoishi Nyabujoli aliishi bibi mmoja mchawi aliyeshindikana Bugwema nzima. Bibi huyu alikuwa akiroga kwa kushirikiana na mwanaye aliyekuwa akiishi naye. Mwanaye huyo hakuwa na mke. Pamoja na kwamba alikuwa mchawi yule bibi alimpenda sana Nyabujoli, sana sana kutokana na upendo na wema wake kwake na kwa wengine. Mara nyingi Nyabujoli alimfanyia kazi yule bibi; kama vile kumtekea maji, kumpikia, kumfulia, na kumsafishia nyumba, pasi na kuombwa.
 
Yule kijana, mtoto wa yule bibi, naye alimpenda sana Nyabujoli. Alimpenda kiasi cha kutaka kumuoa. Lakini Nyabujoli hakuwa tayari kuolewa naye.
 
Yule kijana alipoona imeshindikana alimshauri mama yake wamchukue Nyabujoli kichawi ili amuoe akiwa msukule. Lakini bibi, kutokana na wema wa Nyabujoli, akakataa katakata Nyabujoli kuchukuliwa kichawi na kuolewa kwa nguvu.
 
Jitihada za kumuoa kihalali ziliposhindikana yule kijana alilazimika kumchukua Nyabujoli kichawi, kwa kutumia mamba wawili aliokuwa akiwafuga yeye na wazazi wake. Mama yake kusikia hivyo akatishia kumshtaki mwanaye katika baraza la wanangwa, lakini kijana hakumsikiliza mama yake. Hivyo, akaendelea na harakati zake za kichawi dhidi ya Nyabujoli.
 
Siku mbili au tatu baada ya hapo yule kijana alidhamiria hasa kumuoa Nyabujoli kwa namna tofauti kabisa na ilivyozoeleka. Jioni moja, alipotoka ziwani kuvua samaki na kuogelea, aliingia chumbani mwake na kujifungia humo. Mama yake alikuwa msibani katika kijiji cha jirani na alitarajia kurejea kesho yake.
 
Chini ya uvungu wa kitanda chake kulikuwa na mamba wakubwa wawili. Mamba hao, waliokuwa wamekuja kula kutokea katika maskani yao katikati ya kisiwa cha Kaguru na kisiwa cha Nyamasange, aliwafuga toka wakiwa mijusi hadi wakawa mamba wakubwa kabisa kwa kuwachanja kwa dawa za kichawi.
 
Kwa ishara yule kijana aliwaita wale mamba na kuwatayarisha kwa ajili ya tambiko la kumroga Nyabujoli; ili baadaye, kesho yake asubuhi, aweze kumchukua katika mazingira ya kutatanisha. Alivaa kaniki kisha akachukua mikoba yake yote ya kichawi, kisha akachukua punje za mahindi alizozihesabu hadi kufikia 108. Yote haya ni kwa mujibu wa kijana mwenyewe alipoitwa kwenye baraza la wanangwa kwa ajili ya mahojiano na kukiri makosa yake.
 
Wale mamba wakimwangalia kwa utulivu, yule kijana alitamka sentensi fulani nzito katika lugha ya kichawi mara 108: “Om ah niti ya, Nyabujoli, lufu la suaha”, ambayo ni lugha ya Kibuda. Maneno hayo, katika hali ya kawaida, huweza kumgeuza mtu nguruwe ndani ya siku saba.
 
Wakati akitamka maneno hayo yule kijana alikuwa akidondosha kitandani zile punje 108 za mahindi, moja baada ya nyingine, mpaka maneno yote 864 yalipotimia. Hapohapo Nyabujoli akiwa nyumbani kwao akatamani kwenda ziwani kesho yake asubuhi, kwa ajili ya kuosha vyombo walivyovitumia usiku.
 
Kabla mama yake hajarudi kutoka msibani, yule kijana alitoka nje na kumwita binti wa jirani aliyekuwa akiroga naye na aliyekuwa rafiki mnafiki wa Nyabujoli. Kisha alimpa yule binti dawa ya unga ili kesho yake asubuhi aende akamguse Nyabujoli begani, kirafiki, nyumbani kwao, kisha arudi upesi ili ampe dawa nyingine ya kumuondolea uchawi.
 
Yule binti alivyomgusa tu Nyabujoli begani, kesho yake asubuhi, hapohapo Nyabujoli aliingia ndani akiwa amevaa kaniki na kuchukua vyombo ili awahi ziwani kuvisafisha. Wakati Nyabujoli akielekea ziwani, yule binti alirudi haraka kwa yule kijana ili wamalizie uchawi kabla ya saa sita mchana.
 
Harakaharaka waliwatoa wale mamba wawili na kutembea nao kuelekea ziwani huku wamewashika mikia ili watembee kwa urahisi. Walipofika ziwani, wale wachawi waliwaruhusu mamba kuingia majini; nao mamba wakaogelea kwa fujo na kasi kubwa, kuelekea mahali alipokuwa Nyabujoli.
 
Nyabujoli akiwa peke yake ziwani, isipokuwa mzee mmoja aliyekuwa akipita kwa mbali, aliingia ndani ya maji ili ateke maji masafi zaidi kwa ajili ya kusuuzia vyombo. Lakini ghafla, kabla hajachota maji ya kutosha katika ndoo, waliibuka mamba wawili wakubwa. Mmoja alimmeza Nyabujoli, miguu chini kichwa juu, kiwiliwili kikiwa ndani ya mamba lakini kifua na kichwa vikiwa nje, kwa fujo na kutokomea naye ziwani, huku yule mwingine akiwalinda wote na kumsindikiza mwenzake.
 
Yule mzee aliyekuwa akipita kwa mbali aliushuhudia mkasa wote kwa macho yake. Kuona hivyo akakimbia hadi kijijini na kutoa taarifa kwa watu wote, kwamba Nyabujoli alimezwa na mamba.
 
Mamba walizunguka kisiwa na kwenda mbali zaidi kama vile wanakwenda Uganda lakini wakapumzika katika kichaka cha magugu maji (‘olutende’), ambapo kumbe ndipo yalipokuwa maskani ya mamba wale pamoja na mamba wengine zaidi ya kumi waliokuwa wakifugwa na baba yake yule kijana. Mamba aliyemmeza Nyabujoli alimtapika na wakakaa naye hapo hadi usiku, ambapo mamba alimmeza tena Nyabujoli, na safari ya kuelekea kwa yule kijana mchawi ikaendelea.
 
Katika upande mwingine wa kisiwa yule kijana na yule binti walikuwa wakisubiri. Mamba walipofika, yule aliyemmeza Nyabujoli alimtapika. Nyabujoli alikuwa amechoka sana. Hata hivyo, walimkokota hivyohivyo hadi nyumbani kwao na yule kijana ambapo, kwa bahati mbaya sana walikuta mama yake amesharejea kutoka msibani. Bibi kuona hivyo, alivyoona ni Nyabujoli, palepale alimwambia mwanaye amrudishe mtoto wa watu. Kijana alikataa kwa nguvu zake zote. Lakini mama akazidi kukasirika na kutishia kumshtaki katika serikali ya mtemi.
 
Nyabujoli aliingizwa ndani, akapewa chakula, akanyweshwa na kuchanjwa dawa za kumfanya msukule; huku wale mamba nao wakipewa chakula na kuondoka kuelekea kwenye kichaka cha magugu maji, walipoishi na wenzao.
 
Kifo cha kimazingara cha Nyabujoli ulikuwa msiba mkubwa sana kijijini Bugwema. Asilimia kubwa ya watu walimlilia sana Nyabujoli. Kwani hakustahili kifo cha namna ile.
 
Hata hivyo, watu wakiwa msibani siku ya pili ya matanga, saa tisa usiku, nyumbani kwao Nyabujoli, kuna jambo la ajabu sana lilitokea. Mamba wawili, akiwemo yule aliyemmeza Nyabujoli ziwani, mmoja wao alimtapika Nyabujoli. Kisha Nyabujoli, akionekana kuwa na akili punguani lakini akionekana kuchoka, alitembea kwa kunyata hadi dirishani kwa mdogo wake na kumwita ili amfungulie dirisha. Alikuwa akihitaji chakula.
 
Wanaume kama hamsini hivi walikuwa wamelala nje, huku wanawake wengi pia wakiwa wamelala ndani ya nyumba tatu za nyasi.
 
Mdogo wake alivyopiga kelele kwa kumwona Nyabujoli, Nyabujoli alikimbia lakini akamezwa tena na mamba na kutokomea majini.
 
Kuona hivyo watu wakaamini kumbe Nyabujoli alichukuliwa kichawi. Hivyo, harakati kamambe zikaanza hapohapo kumrudisha akiwa hai.
 
Nyumbani kwa yule bibi mchawi hakukukalika. Bibi alizidi kumsisitiza mwanaye amrudishe Nyabujoli nyumbani kwao. La sivyo angemripoti serikalini na serikali ingemfungulia mashtaka.
 
Jitihada za bibi zilipoonekana kushindikana, alifunga safari hadi nyumbani kwao Nyabujoli. Alikuwa na lengo la kuongea na Mkwaji, mama yake Nyabujoli, lakini roho yake ikasita; hivyo akaamua kumwambia jirani, rafiki yake Mkwaji, kuwa wasiendelee kuomboleza kifo cha binti yao mpendwa, kwani Nyabujoli waliyemlilia alikuwa nyumbani kwake kama msukule wa mtoto wake.
 
Watu kusikia vile wakawa na hamu ya kumwona Nyabujoli akiwa hai. Siku nne baada ya Nyabujoli kumezwa na mamba, yule bibi mchawi alichukua baadhi ya watu usiku akawapa dawa na kuwaomba awapeleke wakamwone Nyabujoli.
 
Walipofika nyumbani kwa bibi, majira ya saa tatu hivi za usiku, wale watu walishuhudia mamba akimtapika Nyabujoli na kukimbia kurudi katika kichaka cha magugu maji walikotokea.
 
Nyabujoli alipotaka kukimbia kuwafuata mamba walimdaka kwa nguvu na kumbeba juujuu hadi nyumbani kwa yule bibi, huku Nyabujoli akipiga kelele akitaka aachiwe, ambapo kijana alikuwa akitayarisha chakula kwa ajili ya mamba na kwa ajili ya Nyabujoli.
 
Kijana alipotaka kuleta purukushani alidakwa kwa mikono ya watu wenye nguvu kisha akalazimishwa kumpa dawa Nyabujoli, kiuasumu cha dawa za misukule, ili arudie hali yake aliyokuwa nayo mwanzo kabisa kabla ya kumezwa na mamba.
 
Jitihada za bibi na wale watu aliowapa dawa ya kumwona Nyabujoli zilizaa matunda. Kijana alisalimu amri na kumrudisha Nyabujoli katika hali yake ya kawaida.
 
Nyabujoli alivyoonekana kwao watu wote waliamka na kupiga kelele. Nyabujoli naye alipiga kelele. Aliwahurumia waombolezaji wa msiba wake ambao bado walikuwa wengi, pamoja na kwamba matanga yalishavunjwa.
 
Kulipopambazuka, kesho yake, watu waliyaona waziwazi majeraha ya Nyabujoli katika sehemu mbalimbali za mwili wake. Alikuwa na majeraha mgongoni, kwenye mabega na kwenya mbavu, na sikio lake la kulia lilinyofolewa katika harakati za kumezwa na kutapikwa na mamba.
 
Baadaye Nyabujoli aliolewa na mvuvi maarufu wa Butimba, Mzee Bwire Mtakama Machumu Makunja, aliyekuwa kaka yake mtoto wa mama yake mkubwa, baba yake bibi yangu Martha Maregesi, lakini wakaachana baada ya ukoo kutengua ndoa yao; na akarudi Chiamato, Ukerewe; ambapo alifariki, akiwa mzee, mwaka 1978, bila kurogeka.
 
Wema, ukweli, upendo, furaha, amani, uvumilivu, fadhili, uaminifu, na imani vitakuweka huru dhidi ya uchawi. Ukiwa mwema mchawi ataona aibu kukuroga, hivyo kupelekea asikuroge kabisa, au hata akikuroga usirogeke; ukiwa mkweli juu ya ubaya wake kwake atakuogopa. Ukiwa mwaminifu, mvumilivu na mwenye moyo wa kusaidia watu atakuheshimu; na ukiwa na imani hatakuona.
 
“Zingatia jambo moja muhimu kuwa hatua ya kwanza ya mtu kudhurika inaanzia kwenye hofu ambayo hukuzwa na mawazo yake mweyewe. Ni mawazo yanayompa mhusika shaka juu ya matendo yake binafsi ayafanyayo mbele ya wenzake. Atendaye wema anajiamini zaidi moyoni kuliko atendaye mabaya. Huu ni ukweli.
 
Siku zote mtu mwenye upendo hawezi kuhofu kutendewa mabaya na watu aliowatendea wema na kuwapenda. Kuwa na mawazo hayo pekee huweka kinga thabiti ya mwili kukabili nguvu zenye asili mbaya zinazoelekezwa kwake, kwa vile moyo na fikra huwa hazihukumu kwa matendo na hivyo kuondoa hofu ya kulipwa mabaya.” –Mzizi Mkavu
 
Wema ulimponya Nyabujoli dhidi ya uchawi. Alimezwa na mamba lakini hakufanywa msukule. Wema huohuo utatuponya sisi dhidi ya uchawi.
Advertisements
One Comment
  1. Shetani huroga wafuasi wake.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: