Skip to content

Woga Wako Umaskini Wako

05/02/2018

Tanuru la Moto

263. Mbele ya simba simama kidete usitetemeke miguu. Kisha mwangalie machoni bila woga wa aina yoyote ile, hata akikutisha vipi.

Mfalme Nebukadneza alipouvamia mji wa Yerusalemu na kuushinda katika mwaka wa tatu wa utawala wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, aliagiza baadhi ya wana wa Israeli aondoke nao kurudi Babeli, kati ya mwaka 605 na 562 Kabla ya Kristo. Vijana watatu: Hanania, Mishaeli na Azaria (pamoja na Danieli) walichukuliwa katika kundi la kwanza la mateka.

Walipofika Babeli, maili 25 kusini kwa Baghdad ya leo, vijana hao walipewa majina mapya. Hanania aliitwa Shadraki, Mishaeli aliitwa Meshaki, na Azaria aliitwa Abednego.

Shadraki, Meshaki na Abednego mara tu baada ya kufika Babeli walijaribiwa kulingana na imani yao. Lakini walisimama kidete kumtetea Mungu wao, hata mfalme alivyowatisha vipi. Kwa sababu hiyo, Mungu aliwapa maarifa na uelewa wa kila aina ya fasihi na elimu ya Mesopotamia.

Walipoulizwa maswali na mfalme na watu wenye hekima, Shadraki, Meshaki na Abednego walionekana kuwa na akili mara kumi zaidi ya mtu mwingine yeyote yule katika Ufalme wa Babeli. Kwa hiyo, mfalme akapendezwa nao. Akawatunuku vyeo mbalimbali katika jumba la kifalme.

Baadaye mfalme Nebukadneza aliota ndoto ambayo hakuikumbuka. Watu wenye hekima na wachawi wa Babeli waliposhindwa kumfunulia ndoto yake, mfalme aliamuru wauwawe wote lakini wakaokolewa na Danieli. Danieli alimfunulia mfalme ndoto yake, akaitafsiri kabisa, hadi mfalme akaridhika na kufurahishwa naye.

Kutokana na ndoto hiyo mfalme Nebukadneza aliamua kutengeneza sanamu la dhahabu kama mungu wa kuabudiwa. Sanamu hilo lililokuwa na urefu wa futi tisini na upana wa futi tisini na la dhahabu tupu, kwani inasemekana huko Babeli dhahabu ilikuwa nyingi kuliko vumbi, lilikuwa utabiri wa mwanzo wa Ufalme wa Nebukadneza na mwisho wa Ufalme wa Rumi, ambapo hakuna taifa lolote kubwa katika dunia ya leo litaungana na taifa dogo hadi mwisho na mwanzo wa dunia mpya.

Kisha mfalme akatuma watu kukusanya maamiri, manaibu, maliwali, makadhi, watunza hazina, mawaziri, mawakili, na wakuu wa wilaya zote, ili wahudhurie wakati wa kumzindua mungu huyo, mfalme Nebukadneza aliyemtengeneza.

Kutokana na umuhimu wa sanamu mfalme Nebukadneza aliwatahadhalisha watu hao yatapa 100; kuwa yeyote yule ambaye hangesujudu na kumwabudu mungu wa dhahabu, pindi sauti ya panda na filimbi na kinubi na zeze na santuri na zomari na namna zote za ngoma itakaposikika, atatupwa saa hiyohiyo katika tanuru la moto uwakao.

Lakini sauti ya vyombo hivyo iliposikika, Shadraki, Meshaki na Abednego hawakutii amri ya mfalme hata kidogo. Mfalme alipopewa taarifa kwamba Shadraki, Meshaki na Abednego hawakutii amri yake alikasirika sana. Lakini alipowapa nafasi nyingine ili wasujudu na kuabudu, bado Shadraki, Meshaki na Abednego hawakufanya kama mfalme alivyotaka wafanye.

Kitendo hicho hakikuwa kizuri! Mfalme bila kuchelewa alitoa amri ili Shadraki, Meshaki na Abednego watupwe haraka katika tanuru la moto. Saa hiyohiyo walikamatwa na kutupwa katika tanuru, la moto uliowaka mara saba zaidi, kama mfalme alivyoagiza.

Lakini cha kushangaza, Shadraki, Meshaki na Abednego hawakuwa peke yao, na hawakuunguzwa hata kidogo na moto wa tanuru, hadi mfalme akaogopa na kuwaita watoke nje.

Nebukadneza alipogundua kuwa hawakuwa na jeraha lolote la moto, wala hawakunuka moshi wala hawakuwa na dalili yoyote ya kuwa tanuruni, toka siku hiyo akamwamini Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego; na akaamuru ufalme mzima wa Babeli kufanya hivyo. Masanamu zaidi ya 200 yaliyokuwa yakiabudiwa kama miungu yakateketezwa. Huo ndiyo ukawa mwanzo wa Mesopotamia kumwamini Yehova.

Baada ya hapo mfalme aliwapandisha vyeo Shadraki, Meshaki na Abednego katika nyadhifa mbalimbali za kifalme! Walifanikiwa. Ujasiri wao ulifanya wawe matajiri wa mbinguni na duniani.

Katika dunia ya leo mfalme Nebukadneza ni simba; na simba ni Shetani. Shadraki, Meshaki na Abednego ni mimi na wewe. Tanuru la moto uwakao ni shida inayokukabili katika maisha yako.

Tatizo lako hata liwe kubwa kiasi gani, si lako kulipigania. Mwachie Mungu. Kila mtu ana simba wake katika maisha yake, na ana tanuru lake katika maisha yake; lakini hata simba wako awe mkali kivipi, hata tanuru lako likichochewa moto kiasi gani, usitetemeke miguu wala usiogope chochote.

Kama wana wa Israeli waliweza kusimama kidete mbele ya simba na ndani ya tanuru, katika kipindi ambacho watu hawakumjua Mungu nje ya Israeli, mimi na wewe tutashindwa vipi leo?

Kuwa jasiri mbele ya simba na tanuru la maisha yako, kusudi mwisho wa siku Mungu atakapokutofautisha kimaisha, uende zako paradiso. Ukiogopa kushindwa hutashinda. Woga wako ndiyo umaskini wako.

Advertisements
Leave a Comment

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: