Skip to content

Asili na Fasili

Asili

279. Mtu aliyepoteza kila kitu katika maisha yake hana asili wala fasili. Kuwa makini naye. Ana uwezo wa kufanya chochote.

Mtu asiyekuwa na asili wala fasili ni yule asiyekuwa na wazazi wala watoto wala chochote kile katika maisha yake. Si wa kuchezea.

Ujinga ni kutoijua karama yako. Laiti mtu angeijua karama yake angekuwa na kila kitu katika maisha yake.

Ukiijua karama yako utajua kuwa kifo si adui aliyeshindikana, hivyo hakitakusumbua, na utaishi kulingana na kadari ya maisha yako, ukiwa na kila kitu katika maisha.

Kuwa makini na mtu aliyepoteza kila kitu katika maisha yake. Kwa vile hana kitu cha kupoteza, hataona shida kukupoteza.

Advertisements

Adui Tunayepambana Naye ni Profesa wa Saikolojia

Mbinguni

278. Mbinguni, Shetani alikuwa kiongozi wa kwaya. Duniani, anatumia muziki kuteka dunia.
 
Shetani alikuwa mtaalamu wa muziki huko mbinguni. Hakuna aliyekuwa akiimba kama yeye. Huku duniani anatumia utaalamu huo kuteka dunia nzima. Anatumia muziki wa kidunia na muziki wa injili, kusudi binadamu asiende mbinguni.
 
Mwimbaji anaweza kuwa na nia njema kabisa na muziki wake; lakini Shetani akautumia muziki huo kwa siri, hata kama ni muziki wa injili, kusambaza dhambi ulimwenguni kote.
 
Si rahisi kumshinda Shetani. Kumbuka, amekuwepo hapa kwa zaidi ya miaka 6000. Sisi hata miaka 300 hatujafikisha. Yaani, hakuna mtu mwenye umri wa miaka 300 hapa duniani leo. Anatujua kiasi gani? Anatujua sana.
 
Kuwa makini na muziki wa kidunia. Kuwa makini na muziki wa injili. Adui tunayepambana naye ni profesa wa saikolojia.

Makusudi

Makusudi

277. Watanzania wengi wanafanya makusudi angalau wapate chochote.
 
Usifanye makosa kwa makusudi kuvifurahisha vizazi vya leo na kulishibisha tumbo lako na matumbo ya familia yako. Ukifanya hivyo, vizazi vya leo na vya kesho vyenye akili vitakucheka.
 
Kwani ukifanya kosa kwa makusudi wapo watu watakaogundua kuwa umefanya kosa, na hao watu watakudharau, iwapo watagundua kuwa umefanya kosa kwa makusudi, hata kama hiyo dharau hawatakuonyesha hadharani. Lakini, hilo kosa, baadaye, litafanya udharaulike waziwazi wewe na familia yako.
 
Hata kama watu hawaonekani kuziona juhudi zako, fanya kazi kwa bidii na maarifa, kwani, kwa taarifa yako, wanaziona.

Nuru ni Ukweli wa Kiroho

Mwamba

276. Musa asingekufa wana wa Israeli wasingefika Kanaani. Kwa sababu alikuwa tayari kwenda kuzimu ili wenzake waende mbinguni. Musa alikuwa katika nuru. Alimwasi Mungu katika maji ya Meriba, lakini maji yalitoka. Alikubali kumkosea Mungu kusudi wenzake wabarikiwe, na kweli wakabarikiwa. Nuru ni ukweli wa kiroho. Ukiwa katika nuru miujiza itatokea. Jisikie raha kuumia kwa ajili ya matatizo ya watu. Vaa viatu vya yule anayeumia, ili ujue anaumia kiasi gani, kisha msaidie kwa kadiri ya uwezo wako wote.

Sisi wote tunao uwezo wa kufanya miujiza na kweli ikatokea. Kama mtu anaumwa, tunao uwezo wa kusema apone na kweli akapona. Lakini lazima tuwe tayari kuumia kwa ajili ya hao tunaowaombea miujiza, na hao tunaowaombea miujiza lazima waamini kama kweli tunao uwezo wa kuwaombea miujiza hiyo.

Mtu anapoumwa, hata kama si ndugu yako, unaumia kiasi gani kumwona anaumwa? Uko tayari kujitolea kiasi gani kuhakikisha anapona na kurudia hali yake ya kawaida? Kwa nini leo wale wanaofanya miujiza hata kwa kutamka tu jambo likawa ni wachache sana kuliko wale wa kipindi cha akina Ibrahimu, Musa au Yesu? Kwa sababu leo hatuko tayari kujitolea maisha yetu kwa ajili ya watu wengine kupata miujiza.

Miriamu dada yake Musa na Haruni alipofariki huko Kadeshi katika mwezi wa kwanza wa mwaka wa arobaini wana wa Israeli walikosa maji. Miriamu ndiye aliyekuwa baraka ya maji ya wana wa Israeli jangwani, kwani Mungu aliwapa neema ya kisima cha maji popote pale walipopita kwa sababu ya Miriamu. Miriamu alipofariki, baraka hiyo ilifikia kitembo. Hivyo wana wa Israeli wakajikuta hawana maji.

Kwa nini Musa alikaidi agizo la Mungu? Kwa sababu alikuwa na huzuni kubwa juu ya kifo cha dada yake mpendwa na juu ya malalamiko ya wana wa Israeli kuhusu maji na mambo mengine. Kumbuka Miriamu alikuwa na mchango mkubwa sana katika maisha ya Musa. Farao alipotoa amri ya kuua watoto wote wa kiume wa wana wa Israeli, baba yao Amramu alimtaliki mama yao Yokebedi. Mimba ya Musa ilikuwa bado haijatungwa. Lakini ukatili wa Farao ulipozidi, Amramu alisalimu amri na kuwa mateka wa Farao; kama walivyofanya waume wengine wote wa Kiisraeli katika jamii ya Wamisri.

Nabii Miriamu ndiye aliyerudisha moyo wa Amramu nyuma na kukubali kumwoa tena Yokebedi. Hapo ndipo Musa akazaliwa, na hapo ndipo uhakika wa wokovu wa wana wa Israeli ukathibitika.

Baada ya Musa kuzaliwa, mama yake alipomficha katika magugu ya Mto Nile akiwa mtoto mdogo, Miriamu ndiye aliyemlinda na ndiye aliyemshawishi binti wa Farao amchukue Musa akamlee nyumbani kwao.

Kwa hiyo, Musa alikuwa na wakati mgumu wakati Mungu akimwagiza aongee na mwamba ili maji yatoke huku wana wa Israeli wakilalamika bila kukoma. Alikuwa akiomboleza kifo cha mtu wa muhimu sana katika maisha yake, kilichosababisha akose hata uwezo wa kuwaongoza tena wana wa Israeli.

Wana wa Israeli walipoendelea kulalamika kuhusu maji na mambo mengine, Mungu alimtokea Musa na Haruni katika hema. Alimwambia Musa awakusanye watu kisha aseme na mwamba mbele yao, kwamba maji yangetoka na watu na wanyama wao wote wangekunywa.

Musa na Haruni walipofika kwenye mwamba husika, badala ya kuongea na mwamba kama walivyoagizwa, Musa akaupiga mwamba huo kwa fimbo mara mbili, maji mengi yakatiririka kwa kiasi cha ajabu! Fimbo ile haikuwa kwa ajili ya kupigia mwamba, ilikuwa kwa ajili ya kukusanyia watu.

Lakini Mungu akawakasirikia Musa na Haruni. Kwa nini? Kwa sababu waliasi kinyume cha neno lake pale kwenye maji ya Meriba! Mungu alimwambia Musa aongee na mwamba lakini yeye akaupiga mwamba huo, tena akaupiga fimbo mara mbili. Mungu akamwambia Musa na Haruni akasema, kwa sababu hawakumwamini hawangeweza kufika katika Nchi ya Ahadi.

Ukikisoma vizuri kisa cha Musa na mwamba utaona kuwa Musa na Haruni walifanya kosa kubwa la kizembe. Mungu alisema wafanye hiki lakini wao wakafanya kile. Mungu akawaadhibu, lakini akawapa wana wa Israeli baraka ya maji kama Musa na Haruni walivyoomba.

Mungu alikubaliana na kile ambacho Musa na Haruni walifanya ijapokuwa lilikuwa kosa. Maana maji yalitiririka kutoka kwenye mwamba! Kama Musa na Haruni walikosea kwa nini Mungu aliwapa wana wa Israeli muujiza wa maji? Kwa nini hakuwanyima kwa sababu viongozi wao walikosea? Huwezi kumzawadia mtu aliyekosea. Unamzawadia mtu aliyepatia. Kama Musa alikosea kwa nini maji yalitoka?

Kile alichokifanya Musa na Haruni hakikuwa na makosa machoni pa wanadamu; hakikuwa na makosa machoni pa Mungu pia! Lakini mtu mwenye haki yukoje? Mwenye haki ni yule ambaye siku zote yuko tayari kuumia kwa ajili ya watu wengine. Hata kama tendo analotaka kufanya kuwasaidia wengine litamkasirisha Mungu yuko tayari amkasirishe ili Mungu huyohuyo awabariki wengine.

Sisi wote ndivyo tunavyotakiwa kuwa. Tunatakiwa kuwa na upendo usiokuwa na masharti yoyote; na tunatakiwa kuwa tayari kufa kwa ajili ya maisha ya wenzetu.

Upendo usiokuwa na masharti yoyote una nguvu kubwa kuliko ulimwengu wote. Mathalani, uongo ni kitu kibaya. Dini zote zinakataza uongo. Lakini kama itakubidi kuongopa kuokoa maisha ya mtu, uongo ni kitu kizuri. Kwa sababu hakuna kitu kizuri kama maisha ya mtu.

Musa alipiga jiwe mara mbili kwa sababu kuna baadhi ya wana wa Israeli hawakuamini kama maji yangetoka. Kwa sababu hiyo alikuwa tayari kuangamia ili wenzake wabarikiwe.

Utafanya nini kuwasaidia watu wengine hata kama ni kwa gharama ya maisha yako? Utakuwa tayari kufa ili wengine waishi; kama itakubidi hata kuacha kazi yako ili mtu apone acha na atapona kwa ruhusa ya Mungu.

1 Yohana 2:10 inasema, “Yeye ampendaye ndugu yake, akaa katika nuru, wala ndani yake hamna kikwazo.”

Jisikie raha kuumia kwa ajili ya matatizo ya wengine. Vaa viatu vya yule anayeumwa ili ujue anaumwa kiasi gani, kisha msaidie kwa kadiri utakavyoweza. Kama hana damu au figo zake zimefeli, uwe tayari kutoa damu au figo kumsaidia. Ukifika kwenye ngazi hiyo ya upendo, ukiomba muujiza ili mgonjwa apone, anaweza kupona. Si kuomba muujiza ilhali wewe ni mnafiki.

Safiri na Wenzako

MtihaniRange Rover

275. Kufanikiwa ni mtihani!

Kwa nini Range Rover ina viti zaidi ya vitano? Ili dereva asisafiri peke yake. Ukiona umefanikiwa sana au umeshindwa sana katika maisha, ujue kuna kitu Mungu anataka kutoka kwako kwa ajili ya wengine.

Mungu anataka tusaidiane na tushukuru kwa kila jambo kwani yeye ndiye aliyetuumba, na anajua kila kitu kuhusu maisha yetu.

Katika barabara ya mafanikio, usisafiri peke yako, safiri na wenzako.

Tajiri anaweza kupita na gari lake katika kituo cha daladala wakati mvua ikinyesha, na akaona si vizuri kuchukua hata watu wawili akawapa lifti, licha ya kuwa gari lake linaweza kuwa na nafasi ya watu sita! Katika dunia hii ambapo dereva na abiria wote wanaweza kuwa hatari, hilo linaweza kuwa jambo lisilowezekana. Lakini kiroho, huo ni ubinafsi na Mungu hapendi.

Wema usizidi uwezo ni falsafa ya kidunia, haina maana. Wema hauozi ni falsafa ya Kimungu, ina maana.

Kufanikiwa katika maisha kuna changamoto zake na kushindwa katika maisha kuna changamoto zake pia. Lakini maskini ana changamoto nyingi kuliko tajiri. Tajiri msaidie maskini na maskini msaidie tajiri.

Wanunulie Watumwa Uhuru Wao Kupitia CAST

Watumwa

274. Kuna watumwa wengi zaidi mwaka 2018, kuliko kipindi kingine chochote kile katika historia ya dunia. Hii inatisha. Wanunulie watumwa uhuru wao kupitia CAST.

Miaka mia hamsini na miwili baada ya marekebisho ya Kifungu cha 13 cha Katiba ya Marekani (mwaka 1865) na miaka 69 baada ya kupitishwa kwa Kifungu cha 4 cha Azimio la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu (mwaka 1948) kukomesha utumwa na biashara ya utumwa duniani kote, kuna watumwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote ule katika historia ya binadamu: utumwa wa kazi, utumwa wa ngono, na utumwa wa vitisho; zaidi ya watumwa milioni 27.

Leo utumwa unazingatia sana faida kubwa na maisha ya bei nafuu. Si juu ya umiliki wa watu kama ilivyokuwa huko nyuma, lakini juu ya kuwatumia kama vifaa duni kwa ajili ya kutengeneza pesa.

Bei ya watumwa leo ni rahisi zaidi kuliko kipindi kingine chochote kile katika historia. Leo mtumwa anauzwa kwa dola 50. Mwaka 1850 mtumwa aliuzwa kwa pesa ya leo dola 40,000. Toa msaada wako wa hali na mali kwa taasisi inayojishughulisha na ukomeshaji wa utumwa na biashara ya utumwa duniani iitwayo CAST na taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Free the Slaves, kukomesha utumwa na biashara ya utumwa duniani kote.

Swali la Tatizo ni Jibu la Tatizo

Tatizo

273. Jibu la tatizo hupatikana baada ya kujua swali la tatizo. Swali la tatizo ni jibu la tatizo. Si jibu la matokeo ya tatizo.

Kama tatizo ni ukame hutapata jibu la tatizo hilo mpaka ujue kwa nini kuna ukame. Inawezekana sababu ni mvua; inawezekana sababu ni migogoro ya ardhi au vita; inawezekana sababu ni ukataji miti ovyo; inawezekana sababu ni ardhi kukosa unyevunyevu kutokana na kupungua kwa vina vya mito; inawezekana sababu ni madhara ya ongezeko la joto duniani. Vyovyote itakavyokuwa, jibu litapatikana baada ya kujua chanzo cha tatizo.

Swali la tatizo ni kama vile, “Kwa nini moyo umepanuka?” Swali hilo linahitaji jibu sahihi. Inawezekana moyo umepanuka kutokana na figo kufeli, hivyo kushindwa kuchuja maji vizuri, na kwa sababu hiyo maji mengi kurudi kwenye moyo, hivyo kusababisha upanuke, kwa kusababishwa na wingi wa maji kwenye moyo. Kwa hiyo, badala ya kutibu moyo ambao ni matokeo ya tatizo, unatibu figo ambacho chanzo.

Swali la tatizo ni swali linaloulizia chanzo cha tatizo, litakaloleteleza ufumbuzi wa kudumu wa tatizo lenyewe.

Kwa hiyo, kwa kifupi: Jibu la tatizo hupatikana baada ya kujua chanzo sahihi cha tatizo, na kulitatua tatizo lenyewe.

SERIKALI HUPENDA WATU ILIYORIDHIKA NAO

Serikali na Watu

272. Serikali hupenda watu iliyoridhika nao.
 
Mridhishe bosi wako! Kama huna bosi, iridhishe serikali yako.

Mtawala

Taifa

271. Ukishakuwa mtawala wa kitaifa umeua! Ama kwa kujua au kutokujua! Ama kwa kupenda au kutokupenda!

Taifa ni malaika! Taifa ni Shetani! Laana ya mwenye haki ina haki.

Taifa kama lina haki, mwananchi kama ana haki, laana yake ina haki. Lakini kama taifa halina haki, mwananchi hana haki, vilevile laana yake haitakuwa na haki.

Mtawala wa kitaifa anaweza kufanya maamuzi mazito yanayoweza kuleta madhara makubwa anayoyajua au asiyoyajua.

Wananchi (na watawala) wanapaswa kutumia busara na hekima kuyakubali au kuyakataa maamuzi ya viongozi wao, na wawe na hofu ya Mungu, yawe mema au mabaya.

Vilevile, kila mtu, mtawala au mwananchi wa kawaida, anapaswa kuwa na busara na hekima juu ya maamuzi yake. Maamuzi yoyote yale yanaweza kuwa na madhara makubwa kwa mwananchi au taifa.

Kama Watanzania Wamelaaniwa Wamejilaani Wenyewe

Watanzania

270. Watanzania wana tabia ya kumwomba Mungu badala ya kumshukuru.
 
Kama Watanzania wamelaaniwa wamejilaani wenyewe. Wana tabia ya kumwomba Mungu lakini hawana tabia ya kumshukuru, baada ya kupata au kukosa.