Skip to content

Roho Yako

Roho Yako

289. Roho yako inatoka wapi? Ya kwangu inatoka Tanzania. Kwa sababu amani na utulivu ndivyo vitu vya muhimu zaidi katika maisha yangu.

Kila mtu kabla ya kuzaliwa roho yake iliumbwa na Mwenyezi Mungu na kupangiwa nchi itakapozaliwa na kuishi. Katika nchi hiyo Mungu akatanguliza malaika mwema ambaye kazi yake ni kumsaidia mtu mwenye roho hiyo tangu kuzaliwa kwake hadi kufa kwake hadi baada ya hapo.

Lakini Shetani atakapoinasa roho hiyo, kabla mwenye nayo hajazaliwa, ataibadilisha ili izaliwe sehemu nyingine tofauti na pale alipopanga Mungu; ili imtumikie yeye badala ya kumtumikia Mungu.

Kujua uraia halisi wa roho yako, hivyo kuujua uraia wako, lazima ujitambue; lazima ujue kwa nini ulizaliwa.

Mungu akikuweka mahali unapostahili kuwa, kulingana na takdiri ya maisha yako, hakuna mtu mwenye uwezo wa kushindana na kipaji chako.

Ishi mahali unapostahili kuishi.

Advertisements

Kiburi

Kiburi

288. Kiburi ni kiwango cha juu kabisa cha umimi au ubinafsi, na ni sumu ya mahusiano.

Kuwa na kiasi. Usiwe mjinga sana wala usiwe mjanja sana. Ukiwa mjinga sana utapata matatizo, kwa Mungu na kwa wanadamu, na ukiwa mjanja sana utapata matatizo pia, ambayo ni kiburi, kwa sababu mtu mwenye kiburi hawezi kamwe kuridhika na heshima na unyenyekevu anaoupata kutoka kwa watu.

Watu wenye kiburi ni wabinafsi, watu wanaopenda kuheshimiwa na kunyenyekewa, na wanajiona bora zaidi kuliko wengine, wanaopata taabu sana kuomba msamaha. Kiburi si upendo na upendo si kiburi. Dawa ya kiburi si kiburi kingine. Dawa ya kiburi ni upendo na hekima.

Hata hivyo, kuna tofauti kati ya kutokujiamini na kiburi. Mtu anaweza asijiamini na asiwe na kiburi, na anaweza asijiamini na akawa na kiburi.

Wengine wanasema kiburi ni kizuri, kwamba ili umshinde Shetani lazima uwe na kiburi. Lakini kiburi dhidi ya Shetani unakishinda kwa hekima.

Kibiritingoma

Majaribu

287. Umewahi kutongoza mwanamke akajishauri kukukubali badala ya kujishauri kukukataa? Umewahi kutongoza mwanamume akajishauri kukukataa badala ya kujishauri kukukubali? Ndugu yangu, yashinde majaribu.

Sababu kubwa inayofanya mwanamke au mwanamume ajishauri kumkubali mwanamume au mwanamke badala ya kujishauri kumkataa ni nguvu ya uchumi aliyonayo mwanamume au mwanamke anayetongoza. Kumkataa mtu mwenye nguvu ya uchumi ni vigumu sana hata awe mbaya kiasi gani. Maana nguvu ya uchumi haiangalii sura wala umbile la mtu.

Mwanamke anayejishauri kumkubali mwanamume yeyote mzuri au mwenye pesa, au mbaya na mwenye pesa, au mzuri na mwenye pesa, ni kibiritingoma. Yule anayejishauri kukataa ni muungwana.

Mwanamume anayejishauri kumkataa mwanamke yeyote mzuri au mwenye pesa, au mbaya na mwenye pesa, au mzuri na mwenye pesa, ni muungwana. Yule anayejishauri kukubali ni kibiritingoma.

Kuna tamaa ya ngono na kuna tamaa ya pesa. Mwanamume ana tamaa ya ngono na mwanamke ana tamaa ya pesa, na kinyume chake.

Yashinde majaribu yako, kwani nguvu kubwa ya Shetani imejificha katika mafanikio.

Mwanamume kumtongoza mwanamke au mwanamke kumtongoza mwanamume akakubali au akakataa kirahisi, au vinginevyo, ni jaribu ambalo kila mtu anapaswa kulishinda kwa hekima ya Mungu.

Kiungo cha binadamu kinachofanya watu waongezeke hatukupewa ili tukitumie kwa anasa za ulimwengu huu. Tulipewa kwa ajili ya kuongezeka tukiwa katika taasisi rasmi ya ndoa, kama upendo wa Yesu Kristo na Kanisa, na kwa ajili ya starehe ya macho kama ilivyorekodiwa katika kitabu cha mapenzi cha Biblia kiitwacho Wimbo Ulio Bora.

Mungu alipomuumba Adamu na Hawa amri ya kwanza aliyowapa ni kufanya mapenzi, ili waijaze dunia, wakiwa katika taasisi ya ndoa. Hivyo, mapenzi nje ya taasisi ya ndoa ni dhambi inayostahili aibu.

Kitu Kigumu Kuliko Vyote

Kigumu Kuliko Vyote

286. Kitu kigumu kuliko vyote usikikatie tamaa, hasa kile unachojua kikifanikiwa kitasaidia watu wengi, kwani kuna uwezekano kikawa kizuri na chenye manufaa zaidi kuliko vyote.

Unapokuwa unafukuzia ndoto, njia ya kuifikia ndoto hiyo aghalabu huwa ngumu sana; lakini pale inapotimia, ndoto hiyo huwa kitu kizuri kuliko vyote.

Kama kwako msamaha ni kitu kigumu kuliko vyote ni kizuri kuliko vyote ukiumudu, kwani kigumu kuliko vyote ni kizuri kuliko vyote.

Wachawi Huroga Watu Waliolaaniwa na Mungu

Wachawi

285. Wachawi huroga watu waliolaaniwa na Mungu. Ukijiondoa katika laana ya Mungu maana yake ni kwamba umebarikiwa na Mungu. Hakuna mchawi, yeyote, atakayekuroga ukarogeka.

Kujiondoa katika laana ya Mungu ni kuwa rafiki wa kweli wa msalaba wa Yesu Kristo; na Biblia. Kwani Biblia na msalaba havirogeki. Ukiwa msomaji mzuri wa Biblia utajiepusha na balaa zote za laana ya Mungu; zilizogongomolewa msalabani huko Kalvari, Yesu alipolipa gharama ya maisha yake kutununua kutoka kwa Shetani.

Maisha Mkebe wa Hesabu

Mkebe wa Hesabu

284. Maisha ni kama mkebe wa hesabu. Ndani yake kuna talanta saba. Rula hutusaidia kuweka mambo kwenye mstari. Penseli hutusaidia kuwa na malengo katika maisha. Pembetatu hutukumbusha haki na usawa kwa wote. Kipimapembe hutusaidia kujiheshimu na hutusaidia kupata maarifa. Kifutio hutukumbusha kuanza upya pale tunapokuwa tumekosea. Kichongeo hutusaidia kunoa penseli ili tuendelee kuwa na uwezo wa kujiwekea malengo katika maisha. Bikari hutukumbusha kuwa na mipaka katika maisha yetu. Angalia Shetani ameiba talanta gani katika mkebe wa maisha yako, na uirudishe talanta hiyo kwa gharama yoyote ile.

Bikari ikipotea utagombana na watu kila siku, hutakuwa na hekima ya kutenda jambo, kwani hutakuwa na mipaka katika kila jambo utakalolifanya. Kichongeo kikipotea hutafanikiwa katika maisha, kwa sababu hutakuwa na penseli ya kukuwezesha kuweka malengo katika maisha yako. Kifutio kikipotea, ukifanya kosa hutakuwa na uwezo wa kulisahihisha. Kipimapembe kikipotea hutapata maarifa na hutaheshimika.

Pembetatu ikipotea utaandamwa sana na watu wa haki za binadamu na watu wengine wote wanaopenda haki na usawa popote utakapokuwa. Penseli ikipotea hutakuwa na uwezo wa kujiwekea malengo katika maisha yako. Rula ikipotea ujue mambo yako hayatanyooka kamwe. Mkebe mzima ukipotea, hutakuwa na uwezo tena wa kuuona ufalme wa Mungu.

Hivyo, ni jukumu lako kuona ni talanta gani imechukuliwa na Shetani katika mkebe wa maisha yako na uirudishe kabla mlango wa rehema haujafungwa. Kwani mlango wa rehema ukifungwa, huku bado talanta zako hazijarudishwa, roho yako itaandikwa katika daftari la kuzimu na pengine usiokolewe kamwe.

Kufanikiwa Lazima Ushindikane

Kushindikana

283. Kufanikiwa lazima ushindikane.

Kufanikiwa lazima umshinde Shetani. Wale waliofanikiwa kupitia nguvu za giza wamemshinda Shetani, kwa sababu Mungu ameruhusu wafanikiwe. Bila Mungu kuruhusu, hakuna atakayefanikiwa.

Wapo watu nomi waliobobea katika mambo ya giza lakini hawajafanikiwa; wamekwenda kwa wachawi na waganga wa jadi dunia nzima; na wapo watu wengi waliobobea katika mambo ya nuru lakini hawajafanikiwa; wamekwenda kwa wachungaji, mapadri na mashehe dunia nzima. Kwa nini? Kwa sababu Mungu hajaruhusu wafanikiwe. Lazima kuna sehemu wanakosea ndiyo maana Mungu hajawafungulia milango ya baraka.

Mungu anaweza kutumia mafanikio ya Shetani kwa faida ya watu wake. Mathalani, jambazi anaweza kujenga kanisa kwa ajili ya watu wa Mungu na Mungu akalibariki na akambariki jambazi, kwa sababu sifa kuu ya Mungu ni upendo. Jambazi anaweza kwenda kuiba akafanikiwa, wakati mchungaji anaweza kwenda kuhubiri akapata matatizo.

Mamafia wa Amerika ya Kusini na Kaskazini wanafanikiwa katika mambo yao, kwa sababu wanasaidia watu waliosahauliwa na serikali zao. Wanatoa upendo kwa Mungu, kwa kutoa upendo kwa wengine, ijapokuwa walifanikiwa kupitia nguvu za giza.

Katika giza lazima ushindikane, na katika nuru lazima ushindikane pia. Katika giza lazima ushindikane dhidi ya hila za Shetani, kwa kuwa mshirikina kwelikweli; na katika nuru lazima ushindikane dhidi ya hila za Shetani, kwa kuwa mlokole kwelikweli.

Kufanikiwa lazima ushindikane ama katika nuru au katika giza. Ukishindikana katika nuru umemshinda Shetani, ukishindikana katika giza umemshinda Shetani, lakini kwa ruhusa ya Mwenyezi Mungu.

Kubarikiwa, hata hivyo, si ishara ya kusamehewa dhambi. Kubarikiwa ni ishara ya kuwasaidia wengine.

Imani ya Wakristo Wengi Haina Macho

Miungu

282. Imani ya Wakristo wengi haina macho. Wanaamini watu. Wanaamini kile watu wanachokisema, na kukiandika, badala ya kumwamini Mungu. Kumwamini mtu, au kuamini maandishi, badala ya kumwamini Mungu, ni sawa na kuabudu miungu wengine.

Weka akili yako pembeni kwa muda. Usiamini kile mtu anachokwambia, au usiamini kile unachokisoma kwenye vitabu. Lakini yachukue mawazo yao kisha yajaribishe katika mafundisho yako ya kiroho, ambayo tayari unayo, ili ujue kama kweli kile kilichosemwa au kuandikwa kinaleta maana katika maisha yako. Kama kinaleta, uko huru kumwamini Mungu. Lakini kama hakileti, ukimwamini Mungu umemwamini mungu mwingine.

Yesu na waandishi wote wa Biblia waliongea na kuandika kimafumbo, ili Neno la Mungu lijidhihirishe lenyewe kiroho katika mawazo ya mtu. Unaposikia Neno la Mungu kutoka kwa mtu acha lijidhihirishe lenyewe katika mawazo yako, kabla ya kumwamini au kutokumwamini Mungu.

Mungu ni Mkamilifu Milele

Ukamilifu

281. Mungu ni mkamilifu milele. Anaishi katika ukamilifu wa milele. Hivyo, kabla ya uumbaji, aliishi katika ukamilifu, baada ya uumbaji, ataishi katika ukamilifu.

Ukiichunguza sana hii kauli utajua Mungu ni nani. Mungu ni Muumbaji, aliyekuwepo, aliyepo, na atakayekuwepo.

Hapa duniani kuna watu wawili tu: Mungu na wewe! Wengine wote, vingine vyote, wako au viko kisogoni mwako. Nje ya macho yako kuna Nuru. Nuru hiyo ndiye Mungu. Wengine wote, vingine vyote, ni akisi ya taswira ambazo ziko ndani yako; ambazo unatakiwa kuziona nje ili uone umekosea sehemu gani, na uweze kurekebisha dunia yako ya ndani.

Wale wanasiasa wanaotwambia kila siku kuwa tulete mabadiliko duniani wanajisumbua iwapo hawatatwambia tulete mabadiliko ndani ya dunia zetu za ndani kwanza. Ukibadilisha dunia yako ya ndani, utabadilisha dunia yako ya nje.

Yesu ni Mfalme wa wafalme, kwa sababu baada ya muda fulani atarudisha ufalme kwa Baba yake. Mungu ni Mfalme wa milele asiyeweza kuonekana wala asiyeweza kufa, 1 Timotheo 1:17, na haonekani kwa faida yetu wenyewe.

Kwa nini? Kama Mungu yupo, yuko wapi? Kwa nini asijionyeshe ili nasi tumwone? Kama alituumba, kwa nini hatuonani naye uso kwa uso? Kwani tatizo ni nini? Faida ya yeye kutojionyesha kwetu ni nini?

Mungu hawezi kujionyesha kwetu kwa kuwa asili yetu ya ubinafsi itasababisha mtafaruku na matatizo makubwa dunia nzima. Kila mtu duniani kote atamng’ang’ania, atamtamani sana, na hakuna la maana litakalofanyika. Itakuwa kinyume na kusudi la maisha; na kusudi la maisha ni kuishi naye mbinguni kwa furaha ya milele, na hatutaweza kuishi naye mbinguni iwapo tuliishi naye duniani.

Hewa ipo lakini hatuwezi kuiona wala kuigusa. Hali kadhalika, Mungu yupo lakini hatuwezi kumwona wala kumgusa. Matendo yake makuu kwetu ndiyo yanayofanya tuamini kuwa yupo. Mungu akijionyesha kwetu tutakuwa kama watumwa. Tutakwama ndani ya asili yetu, na hatutaweza kamwe kuwa na upendo.

Mungu aliyeumba mbingu na nchi anaitwa Yehova na anaishi mbinguni juu ya nchi yote (Zaburi 83:18). Mungu anaishi juu zaidi ya sayari zote za ulimwengu wa roho, mahali ambapo muda wa duniani haufanyi kazi, katika kiti chake cha enzi kilichoijaza mbingu nzima.

Mbingu ni mbingu za Bwana, Bali nchi amewapa wanadamu (Zaburi 115:16). Kwa hiyo, sisi tunakaa duniani lakini Mungu anakaa mbinguni ambako ndiko nyumbani kwake.

Kaleb na Yoshua walihitimu madaraja 40 ya ufahamu kufika Kanaani. Kumfikia Mungu unahitaji madaraja 125 ya ufahamu.

Mungu anasema katika Isaya 66:1, “Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni mahali pa kuwekea miguu yangu; mtanijengea nyumba ya namna gani? Na mahali pangu pa kupumzikia ni mahali gani?” Anasema tena katika Matendo ya Mitume 7:49-50, “Mbingu ni kiti changu cha enzi, Na nchi ni pa kuwekea miguu yangu; Ni nyumba gani mtakayonijengea? Asema Bwana, Au ni mahali gani nitakapostarehe?”

Kulingana na mafungu hayo Mungu ni mkubwa wa kupindukia. Kiwiliwili chake kiko mbinguni, miguu yake iko duniani.

Lakini Mungu ni nani hasa? Mungu ni Roho (Yohana 4:24) anayeishi katika ukamilifu wa milele, akiwa peke yake katika mbingu ya kwake mwenyewe, huku malaika na viumbe wengine wote wakiwa chini yake.

Kabla ya uumbaji Yehova alikuwa peke yake mbinguni akiishi katika ukamilifu wa milele. Lakini hilo halikumpendeza hata akaamua kuwa na msaidizi kwa ajili ya kazi maalumu ya uumbaji wa malaika na wa ulimwengu mzima. Mzaliwa wa kwanza wa Yehova (Wakolosai 1:15) anaitwa Yesu Kristo; ambaye Mungu alimuumba kwa mfano wako, ili asaidiane naye kumuumba binadamu kwa mfano wao.

Yesu Kristo anaitwa Mwana wa Pekee kwa sababu hiyo, kwa sababu ya kuwa mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote, na anaitwa Neno kwa sababu yeye ndiye Msemaji Mkuu wa Mungu.

Hivyo, Yohana 1:1 inaposema, “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu” inamaanisha kuwa Neno ni Yesu Kristo. Yesu Kristo ndiye aliyekuwako hapo mwanzo (kumbuka Mungu hana mwanzo wala mwisho) naye Yesu alikuwako kwa Mungu naye Yesu alikuwa Mungu.

Yesu ni Mungu kwa sababu yeye ndiye mtendaji mkuu wa Mungu (Mithali 8:30). Yeye ndiye aliyemsaidia Yehova katika kazi yote ya uumbaji. Yesu ndiye aliyeumba malaika kwa niaba ya Yehova, na ndiye aliyeumba mbingu na nchi na wanadamu kwa niaba ya Yehova. Kwa sababu hiyo Yesu akapewa sifa ya uungu, naye akawa Mungu kwa sababu hiyo. Kwa hiyo, kuna Mungu na kuna Yehova.

Yehova ni Mungu kwa sababu ana uwezo wa kuumba. Yesu ni Mungu kwa sababu amepewa uwezo wa kuumba na Yehova.

Ndiyo maana sijawahi kusikia Biblia ikimtaja Yesu kama Yehova. Inamtaja Yesu kama Mungu. Kwa sababu Yesu hawezi kuwa Yehova. Hivyo, wale wanaosema Yesu si Mungu wako sahihi ikiwa wanamaanisha kuwa Yesu si Yehova. Lakini kama hawamaanishi kuwa Yesu si Yehova, Yesu ni Mungu.

Mungu alivyoumba ulimwengu miaka bilioni 14 iliyopita kwa mujibu wa sayansi ya roho ya Kiyahudi, sayansi ya uminyaji, jambo la ajabu sana lilitokea. Mungu ni mkamilifu wa milele na anaishi katika ukamilifu wa milele. Kutokana na umilele huo Mungu alitengeneza mwisho. Aliuminya umilele kwa nguvu kubwa ya ajabu, umilele ukagawanyika na kutengeneza mwanzo na mwisho, katika tukio linalojulikana kisayansi kama Big Bang, na kitendo hicho kikamficha Mungu hadi leo hii.

Ni jukumu letu kama wanadamu kumtafuta Mungu popote pale alipo, kupitia ushirikiano wa myoyo yetu, ili tutengeneze nguvu inaitwa Arvut, itakayoitengeneza na kuirejesha upya roho ya Adamu, itakayotuwezesha kumwona Mungu na kuishi naye milele hata milele.

Ukimjua Mungu utapata Arvut. Kutokana na Arvut kila hitaji lako litajibiwa kwa kadiri utakavyoomba. Arvut maana yake ni upendo.

Usikazie macho madhehebu, kazia macho Maandiko.

Tumejaa Ulaghai, Unafiki, na Utata

Mamilioni ya Watu

280. Mamilioni ya watu wamechepuka katika mahusiano yao. Wengine wameua na imebaki kuwa siri yao. Wengi wanakwepa kodi ya serikali na hawakamatwi. Lakini hatuwezi kumdanganya Mungu. Kwa sababu anatujua hadi ndani ya mioyo yetu.

Mioyo yetu wenyewe hutudanganya kidogokidogo katika kutenda dhambi, wakati mwingine bila sisi wenyewe kujua. Lakini, iamini Biblia, Mungu hawezi kuichukulia dhambi kirahisirahisi! Kwa sababu anaupenda sana uumbaji wake.

Kuna kitu kibaya sana ndani ya mtu. Hilo liko wazi. Biblia inasema chanzo cha matatizo ya mtu ni moyo wake, roho yake, pamoja na uwezo wake wa kufikiri. Tumejaa ulaghai, unafiki na utata. Tunajichezea sisi wenyewe ule mchezo wa kitoto wa kombolela. Yaani, tunajificha na kujitafuta wenyewe, tunawadanganya watu lakini Mungu anatuona.

Labda ni katika mazingira hayo ambapo moyo hufanya kazi yake kwa uharibifu zaidi. Huficha uovu mkubwa wa dhambi unaoendelea kuwa mkubwa, na matokeo yake kuwa mabaya na mazito zaidi. Moyo unatulaghai katika kufikiri kuwa si mbaya, au kwamba Mungu ni mwenye huruma sana kiasi kwamba atapuuza.

Tusipoacha kutenda dhambi, dhambi haitakomeshwa. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kukomesha dhambi katika maisha yake. Usisubiri wengine waikomeshe kabla au kwa niaba yako. Hata serikali haitaweza kukusaidia.

Kuna namna moja tu ya kukomesha dhambi, nayo ni kufunga milango yote ya dhambi baada ya kumkaribisha Mungu katika maisha yako.

Funga milango yako yote ya dhambi na kaa mbali na nyavu zinazowinda watu kabla miguu yako haijanaswa na nyavu hizo.